Jamal Khashoggi: Trump asema CIA haijamlaumu bin Salman kuamuru mauaji ya mwanahabari

Jamal Khashoggi: Trump asema CIA haijamlaumu bin Salman kuamuru mauaji ya mwanahabari
Rais wa Marekani Donald Trump amesema shirika la
ujasusi la nchi hiyo CIA halijahitimisha uchunguzi wake kwa kumlaumu mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kuamuru mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi.
Khashoggi aliuawa Oktoba 2 ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia jijini Istanbul, Uturuki. Wakati wa uhai wake alikuwa mkosoaji mkubwa sera za Saudia hususani mwanamfalme bin Salman. Alikimbilia Marekani mwaka 2017 akihofia usalama wake.
Maafisa wa CIA waliviambia vyombo vya habari vya Marekani kuwa operesheni ya kumuua Khashoggi lazima ilihitaji ruhusa ya bin Salman ili kufanikishwa. Hata hivyo mamlaka za Saudia zinasisitiza kuwa operesheni hiyo ilikuwa haramu na bin Salman hakuwa na ufahamu wowote wa kutokea kwake.

...(CIA) Hawakuhitimisha hivyo," Trump alijibu hivyo mara baada ya kuulizwa kuhusu ripoti ya CIA juu ya mauaji ya Khashoggi.

Kauli hiyo ya Trump ameitoa jana Alhamisi wakati ambapo bin Salman ameanza zira ya kikazi nje ya nchi yake toka Khashoggi alipouawa. Kwa sasa yupo katika nchi ya Falme za Kiarabu (UAE) ambayo ni mshirika mkubwa wa Saudia ndani ya kanda ya Mashariki ya Kati.

Bin Salman pia anatarajiwa kuiwaklisha nchi yake katika mkutano wa mataifa 20 yeneye nguvu kubwa kiuchumi duniani, G20, utakaofanyika mwisho wa mwezi jijini Buenos Aires, Argentina. Ukiachana na bin Salman na Trump, mkutano huo utahudhuriwa pia na viongozi kutoka Uturuki na nchi nyengine za magharibi amabazo zimekuwa zikiishinikiza Saudia kueleza ukweli mtupu kuhusu sakata la Khashoggi.

Wakati huohuo, Ufaransa imetangaza kuwawekea vikwazo raia 18 wa Saudia ambao wanashukiwa kutekeleza mauaji hayo. Watu hao pia wameshawekewa vikwazo na Marekani, Uingereza na Ujerumani.

Hata hivyo, bin Salman hayupo kwenye listi hiyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa amethibitisha.

Rais Trump amesema ataendeleza mahusiano "mazuri" ya kibiashara na kijeshi baina ya Marekani na Saudia
Trump amesema nini?
"CIA wanahisia mbalimbali. Ninayo ripoti yao, na hawajahitimisha, na sijui kama kuna mtu ambaye atakuwa na uwezo wa kuwa mwanamfalme (bin Salman) aliamuru mauaji," amesema Trump.

Mapema wiki hii, Trump alitoa taarifa iliyosema kuwa "kuna uwezekano mkubwa sana" alikuwa anajua kinachoendelea kuhusu mkasa wa Khashoggi.

Katika taarifa hiyo Trump alisema: "Kuna uwezekano kuwa mwanamfalme alijua fika juu ya tukio hili la kutisha - yawezekana alijua, yawezekana hakujua!"

Trump amkingia kifua bin Salman mauaji ya Khashoggi
Trump atakiwa kutoa majibu kuhusu mauaji ya Khashoggi
Hiki ndicho kikosi 'kilichomuua' Khashoggi
Hata hivyo Trump amekuwa mstari wa mbele kusema Saudia ni mshirika mkubwa wa Marekani, na asingetaka kuharibu uchumi wa dunia kwa kuwawekea vikwazo kutokana na mauaji hayo.

Kauli hiyo ya Trump imepingwa vikali ndani na nje ya Marekani. Tayari baadhi ya Maseneta kutoka chama chake cha Republican pamoja na cha upinzaini Democrat wamemtaka atoe ufafanuzi mahususi juu ya uhusika wa bin Salmatn katika mauaji ya Khashoggi

Katika hatua nyengine, gaazeti la Hurriyet la Uturuki limeripoti kuwa Mkurugenzi wa CIA Bi Gina Haspel aliwaambia maafisa wa Uturuki kuwa shirika lake lina mkanda wa sauti wa bin Salman akitoa maagizo kuwa Khashoggi "anyamazishwe" haraka iwezekanavyo.

Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Trump alisema: "Sitaki kuliongelea hilo. Inabidi muwaulize (CIA) wenyewe."

Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini