Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara, Mohamed Mustafa Yusufali aliyetajwa na Rais John Magufuli kuwa alikuwa akiibia Serikali takriban Sh7 milioni kwa dakika pamoja na wenzake wanne.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Novemba 23, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya wakili wa Serikali, Tulia Holela kueleza kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.
“Kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, upelelezi wake bado haujakamilika naomba mahakama kuipangia kesi tarehe nyingine ya kutajwa,” amesema Holela.
Baada ya kusikiliza hoja hizo Hakimu Shaidi ameutaka upande wa mashtaka kufanya bidii katika jambo hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 7, 2018.
Mbali na Yusufali ambaye anakabiliwa na mashtaka 198 peke yake, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na shtaka moja la utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh15 bilioni ni Alloyscious Gonzaga Mandago, Isaac Wilfred Kasanga, Taherali Sujjauddin Taherali na Mohamed Seif.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA
0 Comments