Watuhumiwa katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dkt. Edmund Sengondo Mvungi, wakishuka ngazi baada ya kusikiliza kesi inayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar.
WATUHUMIWA sita wanaodaiwa kumuua aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dkt. Edmund Sengondo Mvungi, leo Novemba 22, mwaka huu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka la mauaji.
Washtakiwa hao wamesomewa shtaka hilo leo na wakili wa Serikali, Lilian Rwetabula, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mbando, ambao ni, Mianda Mlewa (45), Paulo Mdonondo (35), Msigwa Matonya (35), Longishu Losindo (34), Juma Kangungu (34) na John Mayunga (60).
Kesi hiyo mpya ya mauaji namba 6, 2018, inawashitaki watu hao kwa kosa la mauaji ya kukusudia kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Watuhumiwa hao leo asubuhi, waliachiwa mbele ya Jaji Sam Rumanyika wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada upande wa mashtaka kuwasilisha ombi la kuindoa kesi hiyo chini ya kifungu cha 91(1) cha sheria ya makosa ya jinai (CPA).
Hatua hiyo imefikwa baada ya wakili wa serikali, Nassoro Katuga, kuiomba mahakama kufuta kesi hiyo kwa kuwa Mkurugezi wa Mashitka Serikalini (DPP) hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa.
Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nasoro Katuga, iliwasilisha maombi hayo na mahakama ikakubali kuwaachia washtakiwa hao huru. Baada ya kuachiwa huru walikamatwa tena na kupelekwa Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kusomewa mashtaka mapya ya mauaji ya Dkt. Mvungi.
Baada ya kusomewa hati ya mashtaka, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo, kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Kabla ya kuahirishwa kesi hiyo, washtakiwa hao walidai kuwa hiyo siyo kesi mpya; ilikuwa inaendelea kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu mbele ya Jaji Sam Rumanyika lakini upande wa mashtaka wameamua kuiondoa na kuileta upya katika mahakama ya Kisutu.
Pia washtakiwa hao wameiomba mahakama iwaeleze upande wa mashtaka wakamilishe upelelezi kwa haraka kwani hakuna chochote kipya kwa sababu hakuna ushahidi mpya zaidi ya uleule uliosomwa kwenye Committal (maelezo ya mashahidi).
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 6, mwaka huu kwa madai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Sponsored by
ZAMOTO MEDIA
0 Comments