Godzilla Akiri Kuwa Chapombe

Godzilla Akiri Kuwa Chapombe
MIONGONi mwa marapa wakali kwenye gemu la Bongo Fleva kuna jamaa anayekwenda kwa jina la Golden Jacob Mbunda ‘Kingzilla’ au ‘Godzilla’ au ‘Zilla’.  Jamaa huyu alifanya vizuri kwa kipindi kirefu, akichuana na wababe wenzake kunako ulimwengu wa freestyle kama Nikki Mbishi na Wakazi.

Lakini kwa muda sasa, Zilla amepotea kwenye gemu na mambo mengi yamekuwa yakizungumzwa juu yake. Pombe imekuwa ikitajwa kuwa ni chanzo cha yeye kupotea. Mapema wiki hii Amani lilimuibukia Zilla nyumbani kwao, Mbezi-Salasala jijini Dar na kufanya naye mahojiano marefu ya vitu mbalimbali ambavyo watu wengi wanatamani kufahamu kutoka kwake, huyu hapa;

UNAWEZA KUWAKUMBUSHA MASHABIKI WAKO JUU YA SAFARI YAKO KATIKA FREESTYLE?

Godzilla: Nilianza kitambo sana, ilikuwa ndiyo kitu f’lani ambacho mimi ninakipenda tangu nikiwa shuleni.

NI NANI ALIYEKUWA ANAKUSUMBUA KATIKA FREESTYLE?

Godzilla: Hakuna ambaye alikuwa ananisumbua kwa sababu naamini mimi nafanya muziki wangu ambao haufanani na mtu yeyote. Kwa hiyo sijawahi kuwaza kujilinganisha na mtu maana ndiyo mwanzo wa kujua mtu anayekusumbua, jambo ambalo wengi wanafeli.

UKIMYA WAKO UMESABABISHWA NA NINI?

Godzilla: Nipo kimya kwa muda kwa sababu naandaa albam yangu mpya ambayo bado mpaka sasa sijapanga lini nitaitoa inayokwenda kwa jina la 55555. Imebeba nyimbo nyingi nzuri, watu watainjoi muziki mzuri kwa sababu wanajuaga ninachokifanya ninapokuwa nimetulia.

KUMEKUWA NA MANENO KUWA SIKU HIZI UNAKUNYWA POMBE KUPITILIZA NA UPO TU MTAANI, HUNA ISHU, UNALIZUNGUMZIAJE HILO?

Godzilla: Huwezi kumzuia mtu mwenye mdomo kuongea kwa hiyo ndiyo hulka ambayo tunayo especially Watanzania. Kwa watu ambao wanamjua Zilla, ni mtu ambaye anapenda sana kuishi maisha ya kawaida, nakaa kitaa, napiga stori mbili-tatu na washkaji kwa sababu ndiyo wanasapoti kazi zangu, siwezi kuwavimbia, lazima nitafute muda wa kuongea nao na kupata mawazo kutoka kwao. Kuhusu pombe, kila mtu na starehe yake, wengine tukipata mbili-tatu zinatupa vibe la kutoa vitu vizuri, lakini sinywi kupitiliza kama wanavyosema.

KUNA KIPINDI ILISEMEKANA UNA BIFU NA RAPA MWENZAKO, WAKAZI, HIYO IKOJE?

Godzilla: Wakazi ni mwanangu sana, hayo yalishapita na sasa tumekuwa na kuyaacha yapite na ambacho watu hawajui ni kwamba mimi na Wakazi tunawasiliana sana kwa sababu tuna kundi letu ambalo tunacheza wote baskeball, lakini ugomvi ni mambo ya kawaida. Mkiwa mnafanya kazi pamoja kupishana kauli kupo tu.

UNA MPANGO WA KUOA LINI?

Godzilla: Hayo mambo ni mazito jamani siyo ya kukurupuka, uzuri ndoa huwa ni mipango ya Mungu, wakati ukifika unajikuta tu unapata wa kumuoa na unaoa. Kwa hiyo siwezi nikasema nitaoa lini.

NINI SABABU YA KUMWAGANA NA MTANGAZAJI DOREEN?

Godzilla: Ni vitu vya kawaida sana kwa sababu kuna kupishana kauli katika uhusiano na kufikia muafaka wa kila mtu kuendelea na maisha yake. Lakini tuko sawa, hatuna bifu, tunaongea vizuri, yaani kama hakuna kilichotokea na mimi ni mtu wa Mungu sana, naamini katika kusameheana.

VIPI KWA SASA UPO KWENYE UHUSIANO?

Godzilla: Siwezi kusema chochote kuhusu hilo kwa sababu mimi ni mtu ambaye napenda mambo yawe ya siri sana, sipendi kuongelea kuhusu maisha yangu.

UNA WATOTO?

Godzilla: Siyo nina watoto, nina mtoto mmoja tu wa kiume, tena mama yake amenipigia kuwa mtoto anataka pesa kwa ajili ya kununua nguo za sikukukuu.

NJE YA MUZIKI UNAJISHUGHULISHA NA NINI?

Godzilla: Nafanya vitu vingi ambavyo siko tayari kuviweka wazi kwa sababu nawajua Watanzania wenzangu, naweza nikavitaja kwa kuwahamasisha, lakini wao wakasema najisifu, sijui najiona mimi ndiyo mimi, lakini kwa kifupi nina biashara nyingi ambazo zinanisaidia kwa kiasi kikubwa kuendesha maisha yangu.

UNAAMINI KATIKA KIKI?

Godzilla: Siamini katika hayo mambo kwa sababu mimi ni mtu ambaye naamini katika Mungu na kufanya kazi kwa bidii na si vinginevyo, ila kama mtu anaamini katika hayo mambo sawa, kama haamini sawa, siwezi nikakomenti kwa sababu mwisho wa siku kila mtu ana maisha yake.

UMEWAHI KUWAZA KUWA NA LEBO YAKO?

Godzilla: Ninayo na kuna wasanii wengi sana ambao nimeshawasaini, muda si mrefu nitawatambulisha rasmi kwa Watanzania.

UNATARAJIA KUTOA LINI NGOMA KABLA YA KUACHIA ALBAMU YAKO?

Godzilla: Siwezi kusema kwa sababu nitafanya kama sapraizi kwa mashabiki wangu.

UMEFAIDIKA NINI KUTOKANA NA MUZIKI?

Godzilla: Siwezi nikasema kuhusu mafanikio yangu hata siku moja.

KINGEREZA UMEJIFUNZIA WAPI MAANA UNAONGEA CHA NDANI SANA?

Godzilla: Nimesoma shule za kawaida sana wala siyo international na kuna baadhi ya watu wanadhani labda nimesoma nje ya nchi, hapana, ila nilikuwa na mwalimu mzuri sana wa Kingereza anaitwa Mipata, namshukuru sana na bado ninafanya naye kazi. Kuna baadhi ya nyimbo zangu kashiriki pia kwa namna fulani.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini