Mamlaka za uchaguzi nchini Jamuhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC) zimasema huenda uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika siku ya Jumapili ukahairishwa.
Msemaji wa tume ya uchaguzi DRC CENI Jean-Pierre Kalamba ameiambia BBC kuwa uchaguzi huo huenda ukasogezwa mbele kwa siku kadhaa kutokana na kile kinachotajwa kama maandalizi ambayo hayajakamilika.
Mchana wa leo Desemba 20, tume hiyo inatarajiwa kukutana na wanahabari na jambo jilo linatarajiwa kutolewa ufafanuzi.
Mamlaka nchini DRC zapiga marufuku mikutano ya kisiasa mjini Kinshasa
Kwa nini wapiga kura hawaamini mashine za kupigia kura?
Uchaguzi wa DRC umekuwa ukisogezwa mbele kwa zaidi ya miaka miwili sasa, huku rais anayemaliza muda wake Joseph Kabila akishutumiwa kwa kutoa visingizio kadhaa vya kuahirisha uchaguzi ili aendelee kusalia madarakani.
Wiki iliyopita ghala la tume ya uchaguzi liliopo jijini Kinshasa liliteketea kwa moto na kuunguza baadhi ya vifaa muhimu vya uchaguzi, hata hivyo, mamlaka ziliwahakikishia wananchi kuwa moto huo hautaathiri kufanyika kwa uchaguzi.
Mamlaka zilidai kuwa moto uliozuka kwenye ghala la tume ya uchaguzi hautazuia uchaguzi wa Disemba 23.
"Tumewaambia mafundi wetu ya kwamba wafanye juhudi zao zote ili uchaguzi ufanyike Disemba 23, lakini kila wakati tunaangalia wapi walipofika. Kama haiwezekani tunapanga kuongea na wanasiasa ili kuangalia namna gani tutaweza kuahirisha uchaguzi na kuongeza siku nne, saba au 14 na sioni wapi kuna ubaya wakati tunataka kufanya mambo kwenye utaratibu mzuri," amesema Kalamba.
Tanganzo hilo la ghafla linatokea wakati polisi wamemzuia mmojwapo wa wagombea wakuu wa upinzani wa kiti cha urais Martin Fayulu kuzindua kampeni zake katika mji mkuu wa nchi hiyo.
Alipokuwa kizuizini Fayulu ameiambia BBC kuwa hatakubali uchaguzi uahirishwe hata kwa sekunde.
"Hatuwezi kukubali kukubali kuahirishwa kwa uchaguzi kwa namna yeyote ... (rais Joseph) Kabila amefahamu kuwa mimi naitwa mwanajeshi wa raia, ikiwa tarehe 23 hakuna uchaguzi kabila na mkuu wa tume huru ya uchaguzi wanapaswa kuondoka," amesema Fayulu.
Kama kweli uchaguzi utaahirishwa, kuna kila dalili ya kutokea kwa machafuko ya kisiasa na makabiliano kati ya raia na vyombo vya usalama.
Uchaguzi huu ukifanikiwa kufanyika itakuwa ndiyo mara ya kwanza kwa DRC kushuhudia mabadiliko ya uongozi kwa njia ya amani.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA
0 Comments