Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally Agoma Kuzungumzia Sakata la Membe

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally Agoma Kuzungumzia Sakata la Membe
Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amegoma kuzungumzia sakata la waziri wa zamani, Bernard Membe ambaye alimwita kuzungumza naye kabla yakufanyika kwa kikao cha NEC .

Jana Jumanne Desemba 18, 2018 Kikao  hicho cha Halmashauri Kuu ya CCM  kiliketi ambapo pamoja na mambo mengine, kiliwasamehe na kuwarejeshea uanachama  waliokuwa wenyeviti wa mikoa wa chama hicho huku kikimpitisha Abdallah Mtolea kuwania ubunge wa Temeke.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, Dk. Bashiru alisema hawezi kujibu swali lolote linalohusu suala la Membe katika mkutano huo kwa kuwa anatekeleza kile alichotumwa na mwenyekiti wake, kutoa taarifa ya yale waliyokubaliana katika mkutano wa NEC ulioanza juzi na kumalizika jana.

Dk. Bashiru alipokuwa katika mikutano yake mjini Bukombe, Geita Desemba 1, alimwita Membe ambaye pia aliwahi kuwa miongoni mwa waliowahi kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kufuatia taarifa alizodai kuwa zinazagaa katika mitandao ya kijamii, zikieleza nia yake ya kuwania kumpinga Rais Magufuli katika uchaguzi mkuu ujao.

Alisema tangu alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM hajawahi kuonana wala kuwasiliana na Membe, lakini sasa anachukua uamuzi wa kumwita iliazungumze naye kwa kuwa katika kipindi cha nyuma chama hicho kiliumizwa sana na makundi, fitina, uongo na nguvu ya pesa, mambo ambayo kwa sasa hawezi kuyaendeleza.

Hata hivyo, baada ya kuendelea kwa majibizano na taarifa mbalimbali kutokana na hatua hiyo, Dk. Bashiru alimtaka Membe kufika ofisini kwake kabla ya kikao cha NEC kilichofanyika juzi na jana.

Hata hivyo, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa baada ya hapo, iwapo Membe alionana na Dk. Bashiru au laa, japo kuwa alisema mlango ukowazi kufanya majadiliano maalumu kuhusu mambo mengine ambayo hayahusiani na maamuzi ya NEC jana.

Dk. Bashiru pia alikanusha taarifa zilizokuwa zikizagaa katika mitandao ya kijamii kuwa mjumbe wa NEC kutoka Mara, Stephen Wassira alizuiwa kuingia katika kikao hicho jana asubuhi.

Alisema Wassira alihudhuria kikao hicho na alikuwa miongoni mwa watu waliochangia kwa kujiamini na alitoa mchango mkubwa.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini