Mwalimu Amuua mpenzi wake kisha na yeye kujinyonga kisa usaliti

Mwalimu Amuua mpenzi wake kisha na yeye kujinyonga kisa usaliti
Watu wawili wanaodaiwa kuwa katika mahusiano ya kimapenzi, Karoli Domisian  (36) na Regina Temu (29) wamefariki katika mtaa wa Mafumbo, manispaa ya Bukoba mkoani Kagera baada ya mwanaume kumuua mpenzi wake kisha yeye mwenyewe kujinyonga, kisa usaliti wa mapenzi.

Kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba mauaji hayo yamegundulika Desemba 17 saa 11 jioni katika mtaa huo.

Amesema kuwa Regina Temu (29) ambaye ni mkazi wa Kahororo katika manispaa hiyo na mfanyakazi wa kiwanda cha kusindika kahawa cha Tanica alikutwa amenyongwa kwa tai nyumbani kwa Karoli Domisian (36), Mwalimu wa  shule ya sekondari Nyanshenye iliyoko katika Manispaa ya Bukoba, ambapo baada tu ya kutekeleza mauaji hayo, Karoli alijinyonga palepale kwa kutumia kamba ya manila ndani ya chumba chake.

"Ndani ya chumba chake kulikutwa karatasi yenye ujumbe wa maandishi iliyoonekana kuandikwa na mwanaume, kwamba amejinyonga mwenyewe baada ya kumuua mpenzi wake, kutokana na kumsaliti"Kamanda Malimi.

Malimi ameeleza kwamba Regina alikuwa akiishi na dada yake eneo la Kahororo na kuwa aliondoka Desemba 16 mwaka huu saa kumi jioni na kuaga kuwa anakwenda sokoni lakini hakurudi nyumbani.

"Baada ya dada yake kuona hakurudi, kesho yake ambayo ni Desemba 17, 2018 alianza kumtafuta hadi polisi bila mafanikio, lakini ilipofika saa 11:30 jioni aliamua kuongozana na mtu mwingine kwenda kwa hawara wa mdogo wake na baada ya kufika huko ndipo aligundua kuwa mdogo wake ameuawa na kutoa taarifa polisi ambao waliwahi kufika katika eneo la tukio na kukuta marehemu hao na karatasi yenye maandishi hayo".

Kwa mujibu wa kamanda huyo jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini