Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imesema kuwa Leo desemba 19, 2018 itafunga barabara ya Morogoro sehemu ya 'Kimara Stop Over' hadi Temboni Wilayani Ubungo jijini, Dar es salaam.
Hayo yameelezwa leo, kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, ambapo amesema kuwa barabara hiyo itafungwa kutokana na kuwepo kwa sherehe ya uwekaji wa jiwe la msingi la upanuzi wa barabara hiyo.
"Wizara inapenda kuwataarifu kuwa barabara ya Morogoro kesho Disemba 19, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana itafungwa kwa muda kutokana na sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la upanuzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 19.2", imesema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda, hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi itaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA
0 Comments