FAHAMU ILIKOTOKA FM ACADEMIA | ZamotoHabari

Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam
Bendi ya FM Academia ni kongwe katika tasnia ya muziki wa dansi humu nchini. Wanamuziki wa bendi hiyo kwa pamoja wanao uwezo mkubwa wa kumudu kuwaridhisha wapenzi na mashabiki wake popote wapandapo jukwaani kupiga muziki. Safu ya waimbaji na wanenguaji wake huwa kivutio kikubwa ndani ya ukumbi.

Baadhi ya watu yawezekana wakawa hawajuwi historia ya bendi hiyo iliyojizolea sifa lukiki ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. Kwa miaka 16 mfululizo zimekuwa zikitajwa bendi zinazoshika nafasi tatu juu, moja wapo ni bendi ya FM Academia, iliyoitambulisha Tanzania kwa muziki wa dansi wa kizazi kipya.

Chanzo cha bendi hiyo ililianzia kwa Wasanii ambao walikuwa wakifanya kazi katika bendi ya MK Sound, iliyokuwa bendi dada ya MK Group, zikiwa chini ya umiliki wa ndugu ambao hivi sasa ndiyo wanaomiliki kampuni ya African Stars Twanga Entertainments (ASET) Kampuni hiyo hadi sasa inamiliki bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta International’ MK Sound enzi hizo, ilikuwa chini ya uongozi wa ndugu wawili, akiwamo mwenyekiti wake wa ASET, Baraka Msiilwa, ambaye ni kaka wa Asha Baraka ´Iron Lady´ ambaye ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo.

Aliyekuwa rais wa bendi ya FM Academia, Nyoshi El Saadat, alianza kuelezea safari yao, ambapo aliwataja baadhi ya wasanii waliounda MK Sound kuwa ni pamoja na Credo, Liver Hassan, Depichu, Willy Amuli, King Dodoo Le Bouche, Bibie Alembi Moseka, Elystone Angai, Bakunde Desine, Lesave, John Mary na Louis 14.

Alisema, wakiwa na MK Sound, walipewa mkataba wa mwaka mmoja, 1991 hadi 1992. Baada ya mkataba kumalizika 1992, walitimka na kuipa kisogo bendi hiyo na kwenda jijini Nairobi nchini Kenya. Wakiwa jijini humo wakaunda bendi iliyofahamika kwa majina ya Bogoss Musica.

“Tukiwa Nairobi, tuliongeza wasanii katika nafasi za rapa, ambapo tulimchukua Sege Mwila. Katika safu ya waimbaji tulikuwa na Aristote Emerite, Jose Muzungu, Opicha Cloude, King Blase, Nicco Kasongo, Lwigi B52 na Balleaterve.”

Nyoshi alisema mwaka 1997, walirejea nchini huku wakiwa na baadhi ya wanamuziki, ambapo walichukuliwa na mfanyabiashara Felician Mutta. Wakiwa na Mutta, waliongezeka wanamuziki wengine ambao ni Mulemule FBI, wakaongeza safu ya wacheza shoo, wakamchukua mpiga kinanda, Saidi Comorean na rapa Papii Nguza Viking ‘Papii Kocha’.

Mwaka 1999, wakaingia mkataba na Felician Mutta, ambako alianzisha bendi ya FM International. Wakiwa chini ya Mutta, walitamba na albamu za ‘Khadija’, ‘Atomic’ na ‘Omba omba’ ambazo ziliwapa heshima mjini. Mara baada ya mkataba kumalizika, wakabadili jina la bendi kutoka FM International na kuwa FM Academia the Dream Team, wakampata mmiliki mpya kwa wakati huo ambaye ni Hussein Macheni.

Tangu kuanzishwa kwa bendi ya FM Academia mwaka 1997 bendi hiyo imepata kutoa albamu 10, huku ikileta changamoto mbalimbali kwa bendi nyingine za muziki wa dansi nchini ikiwemo Twanga Pepeta ambayo imekuwa ikisuguana na kunyang’anyana mashabiki na FM Academia kwa muda mrefu.

Albamu ya mwisho ya bendi hiyo ilizinduliwa Desemba 2013, huku ikiwa imebeba jina la Chuki ya Nini, katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mzalendo Pub Kijitonyama jijini Dar es Salaam, huku ikisindikizwa na bendi ya muziki wa dansi ya Mashujaa Musica.

Rais wa bendi hiyo Nyoshi El-Saadat aliwahi kuzitaja nyimbo za albamu hiyo mpya kuwa ni ‘Fataki’, ‘Otilia’, ‘Ndoa ya Kisasa’, ‘Neema’, ‘Dai Chako Ulaumiwe’, ‘Maisha’, ‘Madudu’, ‘Miraessa’ na ‘Intro’ ambazo zote zimeshatengenezewa video.

Meneja wa bendi hiyo Kelvin Mkinga alisema bendi hiyo imekumbana na misukosuko mingi kwa kipindi chote, lakini haikuwahi kutetereka. “Tumekutana na misukosuko mingi lakini mpaka leo FM Academia imekuwa ni bendi bora na imejitahidi kuwapa burudani mashabiki wake ipasavyo.” Alisema Mkinga.

Mkinga anasema bendi ya FM Academia ilizindua albamu ya kwanza ya ‘Hadija’ mwaka 1998 kisha ikafuatia ya pili iitwayo ‘Atomic’ mwaka 1999 na mwaka uliofuata wa 2000 bendi hiyo ilizindua albamu ya tatu iliyopewa jina la ‘Prison’.

“Tulizindua albamu tatu kwa mpigo. Lakini tulivyofika mwaka 2001 tulizindua nyingine pia hii ilikuwa ni katika kuhakikisha kwamba tunaufanya muziki wa dansi wa kizazi kipya ukubalike tofauti na ilivyokuwa mwanzo, pia muziki wetu ulikuwa na asili ya Congo hivyo ulikuwa na mashabiki wengi.” Alitamka Mkinga

Mwaka 2001 walizindua albamu ya nne iitwayo Freedom na kufuatiwa na ya tano ya ‘Mpambe Nuksi’ iliyozinduliwa mwaka 2001 na kisha ikafuata ya sita iitwayo ‘Dotnata’ mwaka 2003 kabla ya ‘Dunia Kigeugeu’ iliyozinduliwa mwaka 2006. “Mwaka 2006 tulipozindua albamu ya Dunia Kigeugeu ilifanya vizuri sana, hatukuamua kutoa nyingine haraka kwa kuwa tulikuwa bado tunalinda ubora wa albamu yetu iliyofanya vizuri kuliko zote sokoni,” anasema Mkinga.

Mkinga alisema baada ya hapo bendi hiyo ilikaa kimya kidogo hadi mwaka 2010 ilipozindua albamu mbili kwa mpigo ambazo ni ‘Vuta Nikuvute’ na ‘Heshima kwa Wanawake’, huku mwaka 2013 ikiumaliza kwa kuzindua albamu ya ‘Chuki ya Nini’.

Alisema bendi hiyo ilikutana na vikwazo vingi kutokana na baadhi ya wanamuziki kuondoka na kwenda kujiunga katika bendi nyingine, lakini iliweza kuendelea kusimama kutokana na waasisi wa bendi hiyo kama Nyoshi El Saadat kuendelea kuitumikia bendi hiyo.

“Miaka ya hivi karibuni tulipoteza wanamuziki wengi ambao waliondoka na kwenda kujiunga na bendi nyingine kutokana na kuhitaji masilahi huku wengine wakihitaji kujisimamia wao wenyewe. Wapo wengi walioondoka katika bendi hii lakini mpaka sasa hatuna mpango wa kusajili wanamuziki wapya.

“Uongozi wa bendi hii hauna mpango wa kusajili wanamuziki wapya hivi karibuni, kwani kulikuwa na pengo katika bendi lakini kwa sasa limefunikwa na wanamuziki haohao hivyo limejitosheleza.

Licha ya juhudi kubwa alizozifanya kwa kipindi kirefu za kuweka katika chati ya juu bendi hiyo ya FM Academia, aliyekuwa rais wake Nyoshi El Saadat, hivi karibuni ametangaza kujing’atua katika bendi hiyo.

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini