FRED NDALA KASHEBA ILIZICHARAZA NYUZI DAZANI | ZamotoHabari

Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam
Historia ya muziki humu nchini haiwezi kumuweka kando aliyekuwa bingwa wa kulicharaza gita la nyuzi 12 Fredy Ndala Kasheba.

Alionesha makali yake hususa alipokuwa katika bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS) na baadaye kwenye benzi ya Zaita Muzica. Pamoja na kulikung’uta gita hilo la nyuzi dazeni, alikuwa kiongozi wa bendi pia alibarikiwa vipaji vya kutunga na kuimba.

Akiwa katika bendi hiyo ya OSS, alibuni mtindo wa Dukuduku aliokuja kuwa maarufu kila pembe za jiji hilo la Dar es Salaam. Baadhi ya nyimbo zake alizotamba nazo ni pamoja na ni Marashi ya Pemba na Kesi ya Khanga.

Kasheba hatunaye tena humu duniani kawa kuwa ni kama ada kwa kila mwanadamu kuiacha dunia. Alipatwa na maradhi yaliyopelekea kifo chake Oktoba 22, 2004 jijini Dar es Salaam akiwa na miaka 58.

Wasifu wake.

Fred Ndala Kasheba aliyeyaanza maisha baada ya kuzaliwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwaka 1946. . Wasifu wa Kasheba unaeleza kuwa alianza kufundishwa gita na baba yake wakati akiwa na umri wa miaka 12.

Baba yake alikuwa anajuwa kupiga gitaa japo hakuwa mwanamuziki. Alikuwa akipiga gita nyumbani kwake baada ya saa za kazi. Moja ya bendi maarufu ambazo zilimtambulisha sana Fredy Ndala Kasheba ilikuwa Orchestra Fauvette.

Bendi hiyo ilikuwa na watunzi na waimbaji mahiri akina Baziano Bwetii na Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’. Wakati wa uhai wake, Kasheba aliwahi kueleza kuwa bendi ya Orchestra Fauvette ilianza Juni 07, 1964 katika jiji la Lubumbashi huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Afafanua maana ya jina hilo Fauvette kwa Kiswahili ni ndege aina ya Chiriku aimbae. Bendi hiyo ilikuwa na mwimbaji ambaye waliamini alikuwa anaimba mithiri ya Chiriku, hivyo wakaamua kuipa bendi jina hilo.

Wimbo wa uliotamba wakati huo ulijulikana kwa jina la Camarade ya Nzela, ambao Fredy aliwahi kusimulia kuwa ni wimbo uliokuwa ukizungumzia rafiki wa kukutana nae barabarani au njiani. Jirani huyo mwenye roho iliyofananishwa na sanduku la nguo, ambalo ndani yake huwezi kujua kuna nini.

Pia ulipigwa wimbo Jacqueline ambao ulitungwa na mwenyewe Freddy na kuimbwa kwa umahiri mkubwa na Baziano Bwetii, ambao alieleza kuwa alimtungia mpenzi wake aliyempenda Jacqueline. Wimbo mwingine uliopigwa katika kipindi hicho ni Nono na Kalemie.

Wimbo huo ulitungiwa binti aliyeitwa Nono mkazi wa Kalemie, ambaye alikuwa mpenzi mkubwa wa bendi ya Fauvette. Fauvette iliwahi kufanya ziara hapa nchini na kujikita kwa kipindi kifupi katika ukumbi wa White House Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Miaka hiyo Ubungo ilikuwa mbali sana na mji, hivyo kulikuwa na ajali nyingi za magari na pikipiki zikiwapata wapenzi wa bendi hiyo wakisafiri kutoka kwenye muziki. Busara zikatumika wakati uongozi wa bendi ulipoamua kuhamishia bendi kwenda katika ukumbi wa Mikumi Tours. Ikiwa huko walikuwa wakiporomosha burudani katika siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

Fauvette walikuwa na ndoto ya kuwa bendi bora Afrika, japo hawakufikia huko lakini waliweza kuweka alama kubwa katika historia ya muziki wa Afrika mashariki na Kati. Ndala Kasheba aliweza kuimarisha jina lake zaidi alipolifanya maarufu kupiga gita la nyuzi kumi na mbili, mwenyewe akiliita nyuzi dazani, hasa alipoanza kulipiga kwa mtindo wa Dukuduku akiwa Safari Sound Orchestra.

Baadaye Fauvette ilirejea kwao ambako bendi hiyo ikabadilishwa jina na kuitwa Safari Nkoy. “Safari Nkoy” ina maana ya ‘Chui msafiri’ kwa lugha yetu ya Kiswahili.

Baadea Kasheba alirejea hapa nchini ambako alipitia bendi nyingi hapa nchini zikiwemo za Orchestra Safari Sound, Maquis du Zaire na Tancut Almasi. Ya mjini Iringa. Alikuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi iliyowajumuisha wanamuziki toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania, wakaiita Zaita Muzika.

Wakazi wa jiji la Dar es Salaam hawezi kumsahau Ndala Kasheba, kwa jinsi alivyokuwa akipita katika hoteli kubwa za Kitalii, nyakati za usiku akiwa na kofia kubwa aina ya Pama, akipiga gitaa lake meza baada ya meza akitoa burudani. Baadae akanzisha kundi lake la wanamuziki likaitwa Kasheba group.

Mpenzi msomaji utakuwa unazikumbuka baadhi ya tungo za nyimbo zake zikiwemo za Umbea, Nimlilie nani, Happy Birthday, Cocoa na Dezo dezo. Ubora wa wimbo wa Dezo dezo ulipelekea mwimbaji wa wa bendi ya Soukous Stars Tshala Mwana, kuimba katika mtindo wa aina yake.

Kasheba ‘aliachia’ nyimbo nyingine za Ziada, Chunusi, Takadiri, Marashi ya Pemba, Kimbunga na Yellow Card ambao ulikuwa kama akijitabiria kifo chake. Tutaendelea kukukumbka daima, Mungu aiweke roho yako pahala pema peponi, Amina.


Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini