JESHI LA POLISI SHINYANGA LAKAMATA WAGANGA WA JADI 19 WAKIWA NA NYARA ZA SERIKALI




Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limedai kuwakamata waganga wa Jadi 19 ambao wamekuwa wakipiga ramli chonganishi na kusababisha kuendelea kuwepo kwa matukio ya mauaji ya wananchi ambayo yamekuwa yakitokana na imani potofu za kishirikina.


Hayo yamebainishwa leo Machi 30,2019 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga ACP Richard Abwao, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mkoani hapa.

Amesema katika misako mbalimbali ambayo inaendelea kufanyika na jeshi hilo ili kukabiliana na uhalifu pamoja na kupunguza mauaji yatokanayo na imani potofu za kishirikina, wamefanikiwa kuwakamata waganga hao 19 pamoja na watuhumiwa wengine 16 wakiwa na vitu vya wizi na madawa ya kulevya.

“Waganga hawa wa jadi tumewakamata pia wakiwa na nyara za serikali ambazo hutumia kupigia ramli chonganishi ambayo ni mikia ya nyumbu, ngozi ya kenge, ngozi ya simba, kucha za simba, mayai ya mbuni, kichwa cha kenge, jino la ggiri, pamoja na bundi mmoja ambaye tukimtoa hapa atakimbia,”amesema Kamanda Abwao.

“Pia katika msako mwingine tumefanikiwa kukamata watuhumiwa saba (7) wakiwa na mali za wizi ambazo ni pikipiki 2, mashine 3 za kunyolea saluni za kike, Tv 5, Radio Sabwoofer  5, Deki 5, King’amuzi kimoja, komputa moja, Friji moja, baiskeli 3, pamoja na watuhumiwa wengine tisa (9) wanawake wakiwa na madawa ya kulevya aina ya bangi uzito wa kilogramu 35 na heroine gramu 195,”ameongeza.

Aidha Kamanda amesema watuhumiwa wote hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na watafikishwa mahakamani kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi za Kisheria, ili liwe fundisho kwa watu wengine ambao hawataki kuzitii sheria za nchi.

Pia ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga, kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo kwa kutoa taarifa dhidi ya waharifu, wakiwamo na wanganga wa jadi ambao wamekuwa wakitoa tiba kwa kupiga Ramli Chonganishi, ili mkoa ubaki kuwa salama kwa kudumisha amani na utulivu.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI


Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga (ACP) Richard Abwao akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa juu ya misako ambayo wanaendelea kuifanya ya kukamata wahalifu, wauza madawa ya kulevya pamoja na waganga wa Jadi ambao wamekuwa wakitoa tiba kwa kupiga ramli chonganishi na kusababisha mauaji ya watu wasio na hatia kutokana na imani za kishirikina.Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga (ACP),Richard Abwao akionyesha nyara za serikali ambazo zimekuwa zikitumiwa na Waganga wa Jadi kinyume na Sheria na kutoa tiba kwa kupiga ramli chonganishi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga ACP Richard Abwao akionyesha dhana ambayo hutumiwa na waganga wa Jadi kutibia wateja wao na kupiga ramli Chonganishi inayo sababisha mauaji ya kishirikina kwa watu wasio na hatia wakiwamo wazee.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga ACP Richard Abwao, akionyesha madawa ya kulevya aina ya Bangi Kilogramu 35 ambayo wameyakamata kutoka kwa wanawake 9 waliokuwa wakifanya biashara hiyo zikiwamo na Heroine Gramu 195.

Nyara za serikali pamoja na dhana ambazo hutumiwa na Waganga wa Jadi kupigia ramli chonganishi.

Nyara za serikali pamoja na dhana ambazo hutumiwa na Waganga wa Jadi kupigia ramli chonganishi.

Afisa wa jeshi la polisi akionesha nyara za Serikali pamoja na dhana ambazo hutumiwa na Waganga wa Jadi kupigia Ramli Chonganishi.

Nyara za Serikali pamoja na dhana ambazo hutumiwa na Waganga wa Jadi kupigia ramli chonganishi.

Waandishi wa habari mkoani Shinyanga wakichukua matukio ya wahalifu waliokamatwa na Jeshi la Polisi Mkoani humo wakiwamo na Waganga wa Jadi ambao hutoa tiba kwa kupiga ramli chonganishi inayosababisha mauaji ya kishirikina kwa watu wasio kuwa na hatia.

Waandishi wa habari mkoani Shinyanga wakiendelea na uchukuaji wa matukio.

Vitu vingine vya wizi vilivyokamatwa na Jeshi la Polisi.

TV pamoja na Pikipiki ya wizi ambayo imekamatwa na Jeshi la Polisi SANLG yenye namba za usajili MC 187 BEM.

Vitu vingine kama unavyoona vikiwa vimekamatwa katika msako huo wa Jeshi la Polisi ndani ya siku nne kwa mkoa mzima ambapo zoezi hilo ni endelevu ili kuhakikisha mkoa unabaki kuwa salama.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga (ACP) Richard Abwao, akitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo, kuacha Tabia ya kupenda kwenda kutibiwa kwa Waganga wa Jadi, bali waende kwenye huduma za kiafya kupatiwa matibabu sahihi na siyo kwenda kupigiwa Ramli Chonganishi.

Na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog


Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini