Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)-Taifa, Freeman Mbowe amesema, amekutana na mambo ya kuumiza alipokuwa mahabusu katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam, tangu Novemba 2018.
Akizungumza na wanahabari leo tarehe 15 Machi 2019 jijini Dar es Salaam, Mbowe ametaja changamoto zinazowakabili wafungwa katika gereza la Segerea huku akikazia kuhusu tatizo la wanaofungwa bila hatia.
“Kuna ugonjwa uliopo magereza kwa lugha ya huko unaitwa ‘Burudani’ ambao ni ugonjwa wa ngozi na unaambukiza, chanzo chake ni kunguni na chawa”.
”Segerea kuna mahabusu kati ya 2300 mpaka 2450 lakini uwezo wa gereza hilo ni mahabusu 750, watu wanalala kitu kianaitwa ‘mchongoma’ yaani mnalala kwa ubavu mmoja kwa masaa matatu kisha mnageuka,” amesema Mbowe.
Mbowe ameshauri vyombo vya kutoa haki viweke mikakati ya namna ya kupunguza mahabusu, akidai kwamba vyombo hivyo kama vitapitia vizuri makosa ya mahabusu hao, itagundua kuwa nusu ya wafungwa walioko magerezani hawakustahili kuwepo huko.
”Sisi hatuna tatizo na mifumo yetu ya utoaji haki kwa maana ya mahakama lakini mahabusu wanavyoishi kule magerezani ni kama tayari wote wamehukumiwa na sio watuhumiwa,” amesema na kuongeza;
”Mimi niombe vyombo vyetu vya kulinda na kutoa haki kwa watu vitafakari namna ya kupunguza hawa mahabusu na kama wataamua kupitia vizuri makosa ya watu, watagundua nusu ya mahabusu wanaojaza magereza zetu ni watu ambao hawakustahili kuwepo kule.”
Aidha, Mbowe amedai kuwa, askari magereza wanakabiliwa na ukosefu wa sare huku akisema baadhi yao wanajinunulia sare.
”Askari magereza hawapewi sare bali wanajinunulia kwahiyo ukikuta mjanja mjanja anavaa vizuri ila ukikutana na aliyechoka kachoka kweli kweli, niombe tu wawezeshwe, kazi wanayoifanya kukaa na mahabusu sio ndogo kama tunavyodhani,” amesema Mbowe.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments