Mjumbe Halmashauri Kuu ya CCM Ataja Kilichomuondoa Lowassa CHADEMA Na Kurudi CCM

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Mjini mkoani Iringa, Joseph Mgongolwa amesema kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt.John Magufuli ndiyo iliyomfanya Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kurejea ndani ya chama hicho kutokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
 
Amesema, Rais Dkt. Magufuli ameendelea kujiwekea alama za kihistoria ndani na nje ya Tanzania kutokana na mbinu shirikishi anazotumia kila siku kuhakikisha anatekeleza ahadai alizozitoa kwa Watanzania wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015.
 
Mgongolwa aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Savanah mjini hapa kuelezea namna ambavyo kasi ya utendaji kazi ya Rais Magufuli itakavyozidi kuwaunganisha Watanzania bila kujali itikadi zao.
 
Alisema, Rais Magufuli licha ya kukumbana na vipingamizi vingi kutoka ndani na nje ya nchi katika utekelezaji wa majukumu yake ya maendeleo, bado ameendelea kuonyesha ujasiri wa hali ya juu ndiyo maana matokeo yake yanaanza kuonekana sasa.
 
"Kurejea kwa Waziri Mkuu mstaafu mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa ndani ya CCM si kwa kushinikizwa na mtu yeyote, bali yeye mwenyewe aliona namna ambavyo mheshimiwa Rais Magufuli anavyotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
 
"Miradi ambayo imezidi kuliletea Taifa letu heshima kubwa, pia amekuwa akitatua hatua kwa hatua kero mbalimbali za wananchi,kununua ndege kwa ajili ya shirika letu la ndege,kufufua uchumi wa nchi na kutumia mapato ya ndani ya nchi kufanya mambo makubwa kwa maslahi ya Taifa letu," alisema Mgongolwa.
 
Pia aliwataka wengine warudi nyumbani ili waunganishe nguvu ya pamoja katika kulijenga Taifa.
 
Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa alirejea CCM mwishoni mwa wiki huku akionyesha tangu awali kuguswa na namna ambavyo Rais John Magufuli anavyotekeleza shughuli za maendeleo kwa ufanisi huku akimpongeza.



Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini