BREAKING NEWZZZZ: MAHAKAMA KUU YAAMURU MALI ZOTE ZA DECI ZITAIFISHWE NA SERIKALI | ZamotoHabari.

Na Mwene Said, Michuzi TV
Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeamuru mali zote zinazomilikiwa na Kampuni ya Development Enterpreneuship for Community Initiative (DECI) ikiwamo magari, mali zisizohamishika (nyumba) na Sh.Bilioni 14.3 kutaifishwa kuwa nali ya serikali.

Pia, imemwagiza Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kubadilisha umiliki wa magari kutoka Deci kwenda kuwa ya serikali,  Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP)kuwasilisha maombi mahakamani ili madalali wakawahamishe wananchi wanaoishi kwenye nyumba hizo kuwa za serikari.
Leo Mei 7, 2019 hukumu hiyo imesomwa  mahakamani hapo mbele ya Jaji Stephen Magoiga. Alisema mali zisizohamishika ikiwamo nyumba zibadilishwe majina ya umiliki kutoka Deci kuwa kwa jina la Msajili Hazina.

Jaji alisema akaunti za kampuni hiyo zilizopo, Benki ya Nmb tawi la Msasani, benki ya Community tawi la Uhuru na KCB tawi la Samora wahamishe  Sh. Bilioni 14.3 kutoka kwenye matawi yao kwenda Serikalini mara watakapopokea amri ya mahakama yake.

Alisema baada ya kupitia maombi  ya mlalamikaji (DPP) na utetezi walalamikiwa  Wakurugenzi wa DECI Jackson Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saiguran Ole Loitg’nye na Samwel Mtares, bila kuacha shaka walalamikiwa wameshindwa kuthibitisha kwamba mali na fedha taslimu zimepatikana na chanzo tofauti kampuni hiyo.

"DPP katika maombi yake amewasilisha vielelezo kuthibisha kwamba mali zote zilipatikana kwa fedha za upatu, zilizopatikana kwa njia isiyo halali lakini walalamikiwa hawajawasilisha majibu yoyote yanayopinga maombi hayo au kufafanua upatikaji wa mali hizo tofauti na vielelezo vya mlalamikaji, mahakama yangu inaamuru mali zote zitaifishwe kuwa mali za serikali." Alisema Jaji Magoiga.


Alisema DPP aliwasilisha maombi akitaka kutaifisha mali hizo kuwa za serikali baada ya kubainika kuwa zimepatikana isivyo halali na kwamba ni fedha chafu. Hata hivyo, walalamikiwa hawajawasilisha utetezi kuonyesha kwamba walikuwa na biashara nyingine zaidi ya upatu.

Jaji aliendelea kuichambua hukumu kwamba walalamikaji wameshindwa kujitetea kwamba fedha na mali zote hazihusiani na upatu uliotokana na makusanyo kutoka kwa wananchi bila kuwa na leseni ya kufanya hivyo.

Alisema lengo la DPP si kuitajitisha serikali bali ni kuwataka watu wafuate taratibu na sheria kuendesha shughuli zao.

Walalamikiwa waliwakilishwa na Wakili Majura Magafu.
Mapema mahakamani hapo Magafu akijibu hoja za mlalamikaji  alidai kuwa akaunti zilizowasilishwa na DPP, kati ya hizo moja inamilikiwa na kanisa na ya pili inamilikiwa na mlalamikiwa wa kwanza.


Hata hivyo, hati ya kiapo iliyowasilishwa na DPP hakuna mahali inaonyesha ushahidi kwamba mali zote zimetokana na fedha za ujanjaujanja.

Jopo la mlalamikaji liliongozwa na Dpp Biswalo Mganga akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu Paul Kadushi, Mawakili wa Serikali Waandamizi, Theophil Mutakyawa na Shadrack Kimaro.

Akijibu hoja za walalamikiwa, DPP alidai kuwa walalamikaji walikuwa wanaendesha mchezo wa upatu kinyume cha sheria na kwamba mali zote ni mali ya DECI zinafaa kutaifishwa.

Alidai kuwa fedha na mali hizo zimethibitika kuwa zilitokana na upatu na ndiyo maana Mahakama ya rufaa katika hukumu yake ilimuelekeza kufungua maombo hayo Mahakama Kuu.

Alidai kwamba,Deci haikuwa na shuguli nyingine yeyote  mbali ya kukusanya fedha  na kwamba wajibu maombi hawakuleta ushahidi wa kulinga hilo hivyo   
biashara haramu ya upatu ndiyo ilikuwa kazi yao.


Kuhusu uhusiano wa mali za kanisa na Deci,Dpp Mganga alidai kuwa fedha zilizokuwa katika akaunti ya kanisa zilikuwa za Deci kwasababu wakàti huo hawakuwa na akaunti kwani walikuwa bado hawajakamilisha usajili.

Katika maombi ya msingi, DPP Mganga aliwaailisha maombi hayo mahakamani hapo, akiiomba itoe amri ya kutaifishwa kwa mali za kampuni hiyo yakiwamo magari 11, nyumba na viwanja vinane na fedha ziwe nali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika maombi hayo, DPP anaiomba mahakama hiyo kutoa amri ya kutaifishwa na kuwa mali ya serikali, nyumba namba UKMMD/1237 iliyoko Mwembe Madafu, Ukonga, Dar es Salaam, kiwanja namba 651, kitalu ‘M’ kilichopo Forest area, Mbeya, nyumba iliyoko kiwanja namba 7, kitalu ‘P’  ikiwa na hati namba  033004/23 kilichopo mtaa wa Rufiji, Manispaa ya Mwanza.

Mali nyingine ni ardhi iliyoko katika kiwanja namba 2/283/2 kitalu “E” Mabibo, Kinondoni, Dar es Salaam, kipande cha ardhi ambacho hakijapimwa kilichopo kijiji cha Manyinga, Turiani, Mvomero, Morogoro, kiwanja namba 467 kilichopo kitalu “H” kikiwa na hati ya usajili namba 48170 kilichopo eneo la Tegeta, Dar es Salaam, nyumba iliyoko kiwanja namba MM/19/P kilichopo Manzese karibu na barabara ya Morogoro, Dar es Salaam na nyumba iliyoko katika kiwanja namba KND/MXS/MNM/Z ikiwa na leseni ya makazi namba KND 008337 Kinondoni, Dar es Salaam.

Magari ambayo DPP anaiomba mahakama kutoa amri ya kutaifishwa na kuwa mali ya serikali ni Toyota Premio lenye namba  T 132 AWJ, Toyota Land Cruiser namba T 480 AUP,   Toyota Rav 4 namba T 274 ATQ, Toyota Mark II namba T 676 AYP, Subaru Legacy namba T 682 AUT, Toyota Ipsum namba T 850 AXY, Toyota Ipsum  T455 ADM, Toyota Mark II T 186 AYX, Mitsubishi Pajero  T 852 AAV, Toyota Lande Cruiser T 789 AUX, Nissan Terrano namba T 899 AYU.

Pia, DPP anaomba mahakama kutoa amri ya kutaifishwa kwa fedha zilizoko benki katika akaunti namba 22601601056 iliyoko National Microfinance Bank (NMB), tawi la Msasani  Sh. 12,503,068,647.89.

Fedha nyingine taslimu ni zilizoko katika akaunti namba 000120100000194/1 iliyoko Dar es Salaam Community Bank (DCB), tawi la Uhuru ikiwa na Sh. 1,457,700,462.49 na fedha taslim zilizoko katika akaunti namba 021140019558 iliyoko Kenya Commercial Bank (KCB), tawi la Samora, Dar es Salaam, ikiwa na Sh. 57,933,304.10.
Viongozi wa DECI Arbogast Kipilimba, Jackson Mtares, Samwel Mtares, Dominick Kigedi na Timotheo Saiguran ole Loiting’ye wakiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam. Picha ya Maktaba.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini