Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MSHERESHAJI maarufu nchini, Emmanuel Mathias (34) anayejulikana zaidi kwa jina la MC Pilipili na mwenzake Heriel Clemence (25) wamepandishwa katika kizimbani cha Mahakama ya Hakimu Kisutu kujibu tuhuma za kuchapisha maudhui kwenye mtandao bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Akisoma hati ya mashtaka, wakili wa Serikali Costantine Kakula akisaidiana na Batrida Mushi leo Mei 19,2019 amedai mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando kuwa washtakiwa wanatuhumiwa kwa shtaka moja la kuchapisha maudhui bila kuwa na leseni.
Amedai, MC Pilipili ambae ni mkazi wa Mbezi Beach na Clemence Mkazi wa Kawe wanadaiwa, kati Novemba 17, 2013 na Mei 2, 2019 katika maeneo tofauti tofauti ndani ya jijii la Dar es Salaam kwa kupitia televisheni za mtandaoni inayojulikana kama Pilipili TV bila kuwa na leseni kutoka TCRA.
Hata hivyo, washtakiwa wamekana kutenda makosa hayo na MC Pilipili amekamilisha masharti hayo na ameachiwa kwa dhamana, huku Clemence akishindwa kukamilisha masharti na amerudishwa rumande.
Hakimu Mmbando amesema ili washtakiwa wawe nje kwa dhamana kila mmoja anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho halali ambao watasaini bondi ya sh milioni tano kwa kila mmoja. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Katika kesi nyingine, mshereheshaji, Julius Warioba(23) maarufu kama Mc Warioba, naye amefikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtega kujibu shtaka la kuchapisha maudhi katika Mtandao bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini( TCRA). Warioba anayeishi Ubungo, anadaiwa kuwa, kati ya Januari 2016 na April 30, 2019 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam mshtakiwa Warioba alichapisha maudhui kupitia Televisheni ya mtandaoni ( Tv online) inayojulikana kwa jina Mc Warioba, bila kuwa na kibali kutoka TCRA huku akijua kuwa ni kinyume cha sheria ya Mtandao.
Mshtakiwa amekana shtaka hilo na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo yamemtaka mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua kutoka kwa Mtendaji wa Kata na barua hiyo, ipitishwe kwa Mkurugenzi wa Manispaa, anakotokea mdhamini huyo.
"Mshtakiwa nakupa dhamana ila kesho ulete barua kutoka kwa Mtendaji wa Kata yako na vitambulisho vyako vitazuiliwa hapa mahakamani hadi hapo utakapolea barua", amesema Hakimu Mtega. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika. Kesi imeahirishwa hadi kesho ajili ya mdhamini kuwasilisha barua kutoka kwa Mtendaji wa Kata.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments