Dk. Mpango Aeleza Ugumu wa Fedha | ZamotoHabari.

Makubaliano ya kimataifa yakiwemo yanayotaka Serikali kutoa kipaumbele kwa sekta kadhaa kwa kutenga kiwango fulani katika bajeti, yamebainika ni vigumu kutekelezwa ipasavyo kutokana na uhaba wa fedha zinazopaswa kugawanywa.

Serikali imekiri kuhusu hilo ikisema kazi inayotakiwa kufanyika, ni kujielekeza kuwezesha ukusanyaji na kupata mapato zaidi ili vipaumbele vya kisekta na kitaifa viwekwe vizuri; vinginevyo nchi ikitekeleza maazimio kama inavyotakiwa, baadhi ya sekta zinaweza kukosa fedha.

Miongoni mwa makubaliano ambayo serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango imekiri kwamba mbele ya safari inabidi kujipanga vizuri kabla ya kuyatekeleza, ni pamoja na Azimio la Sadc linalotaka serikali itenge asilimia 20 ya bajeti yote kwa ajili ya elimu.

"Huko mbele tukifika, lazima tutapanga vizuri badala ya kusema tutatekeleza haya maazimio,"alisema Waziri Mpango wakati akijibu hoja za wabunge zinazohusu masuala ya fedha wakati wakichangia bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyopitishwa hivi karibuni.

Katika maoni, mapendekezo na ushauri wa wabunge 116 waliochangia bajeti hiyo, baadhi yao walitaka serikali kuheshimu makubaliano ya kimataifa ikiwamo azimio hilo la SADC.

Ingawa Dk Mpango alikiri kuwa serikali inapaswa kuyaheshimu, alisema licha ya azimio hilo la kutaka itengwe asilimia 20 ya bajeti yote kwa ajili ya elimu, yapo mengine yanayoelekeza utengaji wa sehemu ya bajeti kwa ajili ya sekta kadhaa.

"Ni kweli; lakini yapo maazimio mengine ambayo Tanzania imekubali," alisema Waziri Mpango na kutaja Azimio la Maputo sambamba na sekta na kiwango cha fedha kinachopaswa kutengwa kwenye bajeti.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, azimio hilo linataka serikali kutenga asilimia 10 ya bajeti yote kwa ajili ya kilimo; afya asilimia 15 ya bajeti yote; utafiti asilimia moja ya pato la taifa na asilimia 0.05 ya bajeti kwa ajili ya takwimu.

"Sasa kama maazimio yote haya yatatekelezwa, sekta tatu tu zitachukua asilimia 45 ya bajeti yote. Sasa kipi kitasalia kwa ajili ya miundombinu, ulinzi na usalama, maji na bajeti ya bunge? alisema Waziri Mpango.

Waziri alisema ni muhimu wabunge wakazingatia kwamba pia sekta nyingine ni muhimu kwa maendeleo ya elimu.

Alitoa mfano wa bajeti ya ulinzi na usalama kwamba ni muhimu kwani vijana walioko shuleni watasoma wakiwa wamehakikishiwa ulinzi na usalama.

Vivyo hivyo kwa upande wa bajeti ya afya, maji, miundombinu ya umeme na teknolojia ya habari na mawasiliano."Ni muhimu tuangalie mambo yote hayo, alisema na kusisitiza kwamba kikubwa ni ukubwa wa keki.

Alisema kazi inayotakiwa kufanyika ni kujielekeza kupata mapato zaidi ili vipaumbele vya kisekta na kitaifa viwekewe vizuri. Bunge linaendelea na mkutano wake wa bajeti jijini Dodoma ambako wizara kadhaa zimeshapitishiwa bajeti zake kwa mwaka 2019/20. Miongoni mwake ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo wabunge waliidhinisha na kupitisha bajeti ya Sh trilioni 1.3 kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Mwaka huu unaokaribia kumalizika (2018/19), wizara hii ilitengewa Sh trilioni 1.4 kiasi ambacho kwa kulinganisha na bajeti ijayo, wabunge walitafsiri kuwa bajeti ya elimu imeshuka.

Akizungumzia tafsiri kwamba bajeti ya elimu imeshuka na kwamba bajeti ya maendeleo imekuwa na mserereko wa kupungua, Dk Mpango alisema kwa kuangalia takwimu, ni kweli.

Alisema, Ukiangalia takwimu, zinaonesha bajeti inapungua katika kutoka asilimia 17 ya bajeti yote 2015/16; asilimia 16 mwaka 2016/17 asilimia 15 mwaka 2017/18 asilimia 14 mwaka 2018/19 na asilimia 14 ya mwaka ujao wa fedha.

"Hata hivyo, si kweli kwamba bajeti ya maendeleo imekuwa na mserereko wa kupungua. Ukiunganisha hizi namba unaona kilichopungua ni bajeti ya matumizi ya kawaida na inapungua kwa miaka miwili iliyopita,"anasema.

Ameainisha mwaka 2015/16 bajeti ilikuwa Sh bilioni 3.2 ikaongezeka hadi Sh bilioni 3.7 kwa mwaka 2016/17. Mwaka 2017/18 ndipo ilishuka kidogo hadi Sh bilioni 3.5 na mwaka huu ni Sh bilioni 3.4 huku kwa mwaka ujao (2019/20) ikishuka hadi Sh bilioni 3.1.

Hata hivyo, alisema hali hiyo inatokana na hatua ambazo serikali ilichukua ikiwamo kuondoa watumishi hewa kutoka katika sekta ya elimu na pia uundaji mpya uliofanyika katika taasisi mbalimbali na kuondoa baadhi ya watumishi kutoka kwenye taasisi mbalimbali za wizara.

Waziri alisema ni muhimu wabunge wakatambua mchango mkubwa wa wadau wengine wa elimu nchini na hususani wamiliki wa shule binafsi lakini pia taasisi za dini.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini