Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akikabidhi hundi ya mfano kwa kiongozi wa kikundi cha Walemavu Chacha Marwa wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo kwa vikundi vya Wanawake, vijana na walemavu katika Jiji la Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akitembelea mabanda ya wajasiriamali wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake,vijana na walemavu katika Jiji la Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akiwa na viongozi wa Mkoa na Wilaya ya Dodoma wakati wa hafla ya utoaji mikopo kwa vikundi Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo katika picha na viongozi pamoja na baadhi ya wawakilishi wa vikundi vya wanawake walipata mikopo isiyo na riba toka Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi akitoa taarifa ya utoaji mikopo wakati wa hafla ya utoaji mikopo kwa vikundi katika Jiji la Dodoma
…………………………..
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amezitaka halmashauri zote nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika utoaji wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye walemavu.
Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya mfano yenye thamani ya zaidi ya shilingi bil 1.06 (1,062,500,000) kutoka katika mapato ya ndani ya Jiji la Dodoma kwa mwaka wa Fedha 2018/19 kwa vikundi 201.
Alisema kuwa halmashauri zingine zihakikishe kuwa asilimia 10 ya mapato yao ya ndani inapelekwa moja kwa moja kwenye vikundi vya wanawake na vijana na watu wenye ulemavu ili kuwainua kiuchumi.
“ Jiji la Dodoma limekuwa la mfano katika mambo mengi kuanzia ukusanyaji wa mapato wameongoza katika pato ghafi na leo hii wametekeleza kwa vitendo Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura Na, 290 kifungu 37A na kanuni zake za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019.
Jafo aliongeza: “ Kukusanya mapato ni jambo moja na utoai wa mikopo ni jambo jingine, halmashauri inaweza kukusanya lakini isitoe mikopo hii kwa vikundi, sasa Dodoma wameyafanya yote haya kwa umakini na ufanisi mkubwa niwapongeze Jiji la Dodoma na niwatake Halmashauri zingine waje kujifunza na kuiga mfano wenu mnafanya kazi nzuri.
Wakati huo huo, Jafo ameutaka uongozi wa Jiji la Dodoma kukaa pamoja na wadau kubuni na kuunzisha mradi mkubwa ambao utaweza kuwanufaisha makundi maalumu ambao utatekelezwa na asimilia 10 ya mapato ya ndani.
“Unajua wananchi wetu wanataka kufanikiwa katika biashara na pia wanapendelea biashara kubwa hivyo mkibuni mradi mkawatengenezea vizuri kisha mkawakabidhi kama sehemu ya mkopo itawajenga na kubadilisha maisha yao kuliko kila siku kuwapa fedha ni vyema wakati mwingine mkawapa vitega uchumi,” aliongeza Jafo.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe amesema Jiji la Dodoma pamoja na kutoa mikopo hii wameenda mbali zaidi kwa kuhakikisha wanatafuta vyuo vya kutoa ujuzi na maarifa zaidi kwa wanufaika wa Mikopo ili iweze kuwa na tija zaidi.
Pia alisema katika siku zijazo wanatarajia kutoa vifaa na vitendea kazi vya biashara zao kuliko kuwapa fedha ili kuwaepusha na vishawishi vinavyoweza kutokea kutokana na kushika fedha mkononi.
Naye Mkurugenzi wa Jiji hilo, Godwin Kunambi alisema kuwa Jiji la Dodoma limeanza kutoa mikopo kwa vikundi kuanzia mwaka wa fedha wa 2015/16 hadi Desemba 2018 ambapo jumla ya shilingi 2,434,757,316 ziko kwenye mzunguko wa mikopo ya vikundi.
Aliongeza kuwa kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 2.6 (2,606,645,760) zilitengwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19 huku kiasi cha shilingi 1,796,730,000 kimeshatolea katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2018.
“Fedha za vikundi unazokabidhi leo kiasi cha shilingi 1,062,500,000 zinaifanya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka wa fedha 2018/19 kutoa mikopo ya jumla ya shilingi 2,859,230,000 sawa na asilimia 109.6 ya malengo tuliyojiwekea” alisema Kunambi.
Jumla ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyokwishanufaika na mikopo ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuanzia mwaka 2015/16 mpaka sasa ni 1,020 vyenye jumla ya Wanachama 10,200 vikiwa na mzunguko wa jumla ya shilingi 3,497,257,316.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments