Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi akitoa salamu za Serikali wakati wa kuaga mwili wa Dk. Mengi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli imesema imesikitishwa na kuhuzunishwa na kifo cha aliyekuwa mfayabishara maarufu nchini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Reginald Mengi aliyefariki dunia Mei 2, 2019 akiwa Dubai .
Akitoa salamu za Serikali leo Mei 7, 2019 wakati wa kuaga mwili wa Dk. Mengi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema kwa niaba ya Rais, Serikali na watanzania wote wanatoa pole nyingi kwa familia ya Dk. Mengi, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na kifo cha Dk.Mengi.
"Serikali tunatoa pole nyingi kwa mke na watoto wa marehemu Dk.Mengi na tunamuomba Mungu awape faraja katika kipindi hiki kigumu kwenu na kwa watanzania.Pia tunatoa pole kwa wafanyakazi wote wa kampuni ya IPP kwa kuondokewa na mpendwa wao na mpendwa wetu.Tunatambua upendo wa dhati ambao Dk.Mengi amekuwa nao kwa watumishi wake.Kifo chake ni pigo kubwa kwao.
"Kama ilivyo kwa familia, serikali nayo imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Dk.Mengi.Kifo chake kimekuwa cha ghafla sana kwani aliondoka nchini akiwa mzima na alipofika Dubai amefariki.Baada ya taarifa za kifo hicho, Serikali kupitia Ubalozi wetu uliopo katika nchi za Falmeza Kiarabu ulianza mchakato wa kuhakikisha mwili unarudishwa nyumbani na unafika salama na leo hii uko mbele yetu.
"Ubalozi wetu ulifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha taratibu zote za kuusafirisha mwili zinapatikana na Serikali ilihakikisha mwili unafika kwa wakati. Balozi wa Tanzania katika nchi za Falme za Kiarab Mbarouk Nassoro Mbarouk amefanya kazi kubwa kuhakikisha mwili unarudishwa kwa wakati.Hata hivyo pamoja na majonzi tuliyonayo tunajua kifo ni fumbo kama ambavyo viongozi wote wa dini wamesema , na mwenye kujua fumbo hilo ni Mungu, hivyo tunamuachia yeye,"amesema Profesa Kabudi.
Pia amesema Serikali imeguswa sana na msiba wa Dk.Mengi kwani amekuwa msaada mkubwa katika kujenga uchumi wa nchi yetu na kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania na kwamba uzalendo wake kwa nchi yake uliweza kuvuta wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini.
"Dk.Mengi enzi za uhai wake mara kadhaa ameshauri namna bora ya kujenga uchumi na wazawa kupewa nafasi na kubwa zaidi alikuwa na majawabu ya nini kifanyike. katika Serikali ya Awamu ya tano, Dk.Mengi alikuwa mwenye maono ya kutekeleza kauli mbiu ya Serikali ya viwanda ambapo alikuwa na mkakati wa kuanzisha kiwanda cha magari na ukweli ni kwamba mchango wake kufanikisha Serikali ya viwanda ni mkubwa.
"Serikali inatambua mchango wa Dk.Mengi katika kusaidia wanyonge, watu wenye kipato cha chini, walemavu na watu wenye ulemavu na utaratibu wake wa kukutana na watu wenye ulemavu inadhihirisha upendo wake kwa kada za watu mbalimbali. Tunatambua mchango wa Dk.mengi katika mazingira kwani amekuwa mchago mkubwa katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa na alianzisha kampeni ya kupanda miti katika mlima kilimanjaro,"amesema.
Waziri Kabudi wakati anaendelea kutoa salamu za Serikali, amesema Rais Dk.John Magufuli alizindua kitabu cha Dk.Mengi mwaka jana na kwamba kitabu hicho ni hazina kwani kinafundisha mambo ambayo ameyafanya Dk.Mengi na kupitia kitabu hicho iwe sehemu ya kuwa somo la kusaidia watanzania wengi.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments