Kituo cha kuwatenga wahisiwa wa magonjwa ya mlipuko ikiwamo ugonjwa wa Ebola, kilichopo katika halmashauri ya Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.
*Waziri Ummy Mwalimu atoa tamko rasmi,aelezea hatua ambazo Serikali inachukua
*Ataja mikoa ambayo iko hatarini zaidi na tishio la ugonjwa wa Ebola nchini
*Aelezea namna ambavyo wamesambaza vifaa tiba nchini,utolewaji wa mafunzo ya kukabiliana na Ebola
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
WIZARA ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imetoa tahadhari kwa umma kuhusu uwepo wa tishio la mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini unaoendelea kuripotiwa nchini DRC Congo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani ni kwamba hadi Juni 14 mwaka huu tayari imeripotiwa watu 2108 wameugua ugonjwa wa Ebola na kati ya hao vifo vilivyotokea ni 1,411 na kwamba uwiano wa wagonjwa na vifo katika kila wagonjwa 100 watu 67 wamefariki.
Akizungumza leo Juni 15,2019 akiwa Mkoa wa Mwanza na taarifa kutuma kwa vyombo vya habari nchini, Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kutokana na tishio la uwepo wa ugonjwa huo tayari Wizara ya afya imechukua hatua kadhaa ya kukabiliana na ugonjwa wa ebola.
"Ugonjwa huu pia uneripotiwa kutokea katika nchi jirani ya Uganda katika Wilaya ya Kasese iliyopo upande mwa Kusini Magharibi mwa Uganda.Kwa upa nde wa Tanzania imepaka na Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera ambapo Juni 11,2019 mtoto mwe nye umri wa miaka mitano amethibitika kuugua ugonjwa huo na kwa bahati mbaya amefariki dunia na katika familia hiyo ndugu wengine wawili wamefariki katika nchi ya Uganda," amesema.
Waziri Mwalimu amesema kutokana na tishio la ugonjwa huo nchini Uganda utaona mikoa ya Kanda Ziwa na hasa Kagera,Kigoma na Mwanza iko hatarini zaidi na hivyo Wizara ya Afya imechukua tahadhari ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini.
"Kwangu naona ugonjwa huu unaua watu wengi zaidi na kwa haraka.Sio kwamba Dengue na Kipindupindu haviuwi lakini Ebola kasi yake ya kuua ni kubwa," amesema Waziri Mwalimu wakati anatoa tamko la tahadhari kuhusu tishio la ugonjwa huo.
Akizungumzia zaidi kuhusu Ebola amesema dalili kuu za ugonjwa ni homa kali inayoambatana na kutokwa na damu katika matundu ya mwili yaani pua,njia ya haja kubwa na ndogo,mdomoni,masikioni na machoni hali inayosababisha kifo kwa muda mfupi.
Waziri Mwalim amesema kipindi cha kuonekana kwa dalil za ugonjwa ni kati ya siku mbili hadi 21 baada ya kupata maambukizi na kwamba ugonjwa huo unaenea kwa urahisi sana na haraka kutoka kwa mtu mmoja had mwingine iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa na kugusana na mate ,damu,mkojo,machozi,kamasi,majimaji mengine ya mwilini ikiwa pamoja na jasho au kugumsa mtu aliyekufa kwa ebola.
Pia amesema ugonjwa huo unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa nguo au mashuka ya mgonjwa ya ebola na kueleza kuwa tangu ugonjwa wa Ebola ulipotaarifa kuwapo nchini DRC Congo ,Wizara imechukua na inaendelea kuchukua hatua katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huo nchini kwa kuchukua hatua mbalimbali.
Ametaja baadhi ya hatua inazochukua ni kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huo kupitia kwa makatibu tawala wa mikoa yote Tanzania Bara.Aidha taarifa hiyo imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa(ainisho la ugonjwa)" Fact sheet" ya ugonjwa.
Amesema Dodoso la kujima utayari wa mikoa na wilaya kukubaliana na ugonjwa huu ,muongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli na vipeperushi vinavyoelezea ugonjwa huu.
Pia kuimarisha utaratibu na ufuatiliaji wa ugonjwa huo kupitia kwa wataalam wa afya katika mikoa,wilaya na maeneo ya mipakani na kuimarisha uchunguzi wa wageni wanaoingia nchini kupitia mipaka yetu,ikiwemo kwa kipima joto,
Ameongeza wamefanya tathimini ya kupima utayari wa mikoa na halmashauri katika maeneo iliyoanishwa kuwa hatari zaidi ya kupata ugonjwa Ebola kutoka nchi jirani.Maeneo yanayotakiwa kufanyiwa kazi yameanishwa na jitihada za kuyaondoa mapungufu hayo zinaendelea.
Waziri Mwalim amesema tayari wamepeleka jumla ya seti 3500 za vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya kupitia ofisi za kanda za Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) na kutokana na tishio la sasa wataongeza seti 4000 na kuzipeleka karibu zaidi na wananchi ikiwa ni pamoja na kwenye hospitali zote za mikoa na wilaya kwa ajili ya kujiandaa.Aidha idadi hiyo itaongezeka kutokana na uhitaji .
"Tumeandaa kitini chenye maelezo muhimu ya kukabiliana na Ebola ambapo nakala tete(softy Copy)zimetumwa kwa waganga wakuu wa mikoa na pia tumeendelea kudurufu nakala zaidi ili kuzisambaza kwenye mikoa,wilaya na vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
" Pia tumeendelea kushirikiana na wadau katika kuimarisha sehemu za kuwatenga na kuwahudumia wagonjwa wa Ebola katika Hospitali ya Temeke,Hospitali ya Taifa Muhimbili, Ilemela Mwanza ,hospitali ya Rufaa ya Mawezi kilimanjaro na utaratibu huo unafanyika kwenye mikoa mingine,"amesema.
Amefafanua pia wametoa mafunzo namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kwa watumishi zaidi ya 460 wa sekta ya afya,na 264 kutoka ngazi ya jamii(viongozi wa dini, wanahabari,bodaboda pamoja na watendaji wa vijiji).katika mikoa iliyo na hatari kubwa zaidi ya maambukizi ya ebola hapa nchini.
Amesisitiza mpango huo ni endelevu na idadi itazidi kuongezeka na tayari wameimarisha utambuzi wa ugonjwa Ebola kwa kujenga uwezo hapa nchini hususani katika Maabara Kuu ya Taifa jijini Dar es Salaam ,Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya na Kilimanjaro Clinical Reseach Institute(KCRI) kilichopo Moshi.
Pia amesema usafirishaji wa sampuli kutoka maeneo mbalimbali kwenda kwenye maabara hizo umeimarishwa. Aidha kwa kushirikiana na wadau kutakuwa na maabara zinazohamishika.
"Tumeendelea kutoa taarifa na elimu kwa umma kuhusu kujikinga na maambukizi ya Ebola nchini kupitia vyombo vya habari ikiwa pamoja na kutambua dalili za ugonjwa huo ili endapo ugonjwa utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.Pia Wizara inaimarisha ushirikishwaji wa vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini na inapobidi ili kuongeza tija ya kukabiliana na tishio hili," amesema Mwalimu.
Wakati huo huo amesema Wizara inatoa maagizo kwa mikoa na halmashauri nchini kwa kuhakikisha zinaimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko , na kutoa taarifa za wiki kwa wakati na zile za kila siku pale inapobidi.
Pia imeagiza kuwepo na utaratibu mzuri wa ushirikishwaji wa wadaumbalimbalo wa mikoa na halmashauri na kuwepo mikakati thabiti ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko katika maeneo hayo.
Amesema ili kujikinga na Ebola ni vema kila mmoja wetu akaepuka kugusa damu,mkojo,jasho ,kinyesi,machozi na maji maji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
"Epuka kushughulikia maiti ya mtu aliyefariki kwa ugonjwa ebola : Aidha tunatakiwa kutoa taarifa kwa uongozi wa kituo cha kutolea huduma za afya kwa ushauri .Epuka mila na desturi zinazoweza kuchelewesha mgonjwa kupatiwa huduma muhimu za afya na kupelekea kueneza ugonjwa wa ebola.Pia kuzingatia kanuni za afya na usafi wa mwili
"Kutoa taarifa mapema kwa uongozi wa Serikali na kwa wahudumu wa afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.Kuwahi katika vituo vya huduma za afya pale unapoona dalili za ugonjwa huo ," amesema.
Waziri Mwalimu ameeleza kuwa ni muhimu kuhusisha viongozi wa kata ,mitaa ,vijiji na vitongoji katika kubaini na kutoa taarifa katika vyombo husika pindi abapoonekana kuna mtu ameingia nchini bila kufuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria.
"Kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Wizara na kuepuka kutengeneza taarifa zisizo rasmi na kuzipeleka kwenye mitandao ya kijamii kuhusu ugonjwa .Wizara ya Afya inatoa tahadhari kwa umma kuhusu tishio la ugonjwa wa Ebola ambalo unaendelea kuripotiwa katika nchi ya DRC Congo," amesema Waziri Mwalimu
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments