DC Ndejembi Aahidi kumaliza mgogoro uliodumu kwa miaka 13 ndani ya Siku 10 | ZamotoHabari.

Na Charles James, Michuzi TV

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Mhe Deo Ndejembi amekutana na viongozi wa Kata ya Lenjuru na Kata ya Njoge ili kutatua mgogoro wa mipaka ambao umedumu kwa kipindi cha miaka 13.

Akizungumza baada ya mkutano aliofanya na viongozi wa pande zote mbili Mhe Ndejembi ameeleza kugundua kiini cha mgogoro huo ni maslahi binafsi ya watu ambapo ubavu mmoja unafanya eneo hilo kama malisho ya mifugo yao huku upande mwingine ukiwa umeuza maeneo yao kwa wakulima na hivyo kusababisha mgongano huo.

" Baada ya kusikiliza pande zote mbili nimegundua kuna mgongano wa kimaslahi baina yao, mwanzoni walikubaliana kwamba pande zote mbili zitumie eneo la mpaka kama malisho, hivyo nimetoa maelekezo kwamba kabla ya Julai 30 mwaka huu tukutane tena tukiwa na ramani ya Wilaya na Kata zote mbili ili tuweze kubainisha mpaka huo," amesema DC Ndejembi.

Aidha DC Ndejembi amesema watawapokonya mashamba wale wote waliogaiwa kinyume na taratibu na kuyarudisha kwenye Serikali ya Kijiji baina ya kubaini wapo baadhi ya watu waliogaiwa mashamba hayo kinyume na utaratibu.

" Wale ambao wanamiliki mashamba kinyume na utaratibu wajiandae kuyarudisha, Sheria no5 ya mwaka 1999 toleo la 2002 linasema wazi kwamba Kijiji mwisho wake kutoa ni ekari 50 lakini Kijiji hiki cha Njoge kimempa Mfanyabiashara mmoja mkubwa Ekari zaidi ya Ekari 1200 kinyume na utaratibu na eneo hilo wamemgawia kutoka kwenye eneo la malisho jambo linaloleta mgogoro huu," amesema DC Ndejembi.

DC Ndejembi amesema maamuzi yake kuhusu mgogoro huo yanaenda kwenye ramani ambayo inaonesha mpaka kati ya Kata ya Pandambili na Njoge kwa sababu Lenjuru ilizaliwa kutoka Kata ya Pandambili na Njoge haikuwahi kumegwa, hivyo maamuzi yake ni kwenda kwenye mpaka halisi kwa sababu ilipozaliwa Kata ya Lenjuru hakuna kilichobadilika zaidi ya mpaka uleule uliokuepo.
 Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe Deo Ndejembi akizungumza na viongozi wa Kata za Lenjuru na Njoge katika mkutano wa kutatua mgogoro wa mipaka baina ya Kata hizo mbili uliodumu kwa miaka 13
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe Deo Ndejembi (katikati) akijadiliana jambo na viongozi wa Kata za Lenjuru na Njoge baada ya kumaliza nao mazungumzo yaliyolenga kutatua mgogoro baina yao uliodumu tangu mwaka 2006


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini