Mbunge Ditopile amwaga mifuko 100 ya saruji UVCCM Ruvuma | ZamotoHabari.


Na Charles James, Michuzi TV

Mbunge wa Viti Maalumu Taifa anayewakilisha vijana, Mhe Mariam Ditopile amechangia mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya Shilingi Milioni Moja na Laki Sita Kwa ajili ya kujenga Hosteli za Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi UVCCM mkoani Ruvuma.

Mhe Ditopile ametoa mifuko hiyo ya saruji wakati aliposhiriki shamrashamra za Ruvuma ya kijani na kutekeleza ombi la vijana wa Mkoa huo waliomuomba kutoa mchango wake kwa ajili ya Hostel hizo ambazo zitatumika kama kitega uchumi cha UVCCM mkoani humo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo ya Ruvuma ya kijani Mhe Ditopile amempongeza Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Ruvuma, Raymond Mhenga kwa maandalizi mazuri pamoja na uthubutu wao kama vijana wa ujenzi wa Hosteli hizo ambazo zitaimarisha uchumi wa Umoja huo.

" Nitumie fursa hii kuupongeza Uongozi wa UVCCM Ruvuma chini yake Comrade Mhenga, tunaposema uchumi wa kati ni pamoja na Umoja wa vijana, hivyo nimetoa mifuko hii 100 ya saruji ili kuhakikisha hostel hizi zinakamilika na kuwa sehemu ya kitega uchumi cha UVCCM.

" Mimi kama Mbunge naetokana na Umoja huu na kuwakilisha vijana nawaahidi ushirikiano na kuwa nanyi bega kwa bega, tupeane ushauri na kusaidiana kwa pamoja leo likiwa ni kumuunga mkono Mhe Rais Dk John Magufuli katika kuwatumikia wananchi wetu, "amesema Mhe Ditopile.

Nae Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Ruvuma, Raymond Mhenga amempongeza Mhe Ditopile kwa kazi kubwa anayofanya katika kuwatumikia Watanzania Nchi nzima hasa vijana na kumuomba kuendelea kushirikiana na Umoja huo katika kila kujenga Tanzania yenye uchumi wa kati.
 Mbunge wa Viti Maalum Taifa anayewakilisha Vijana, Mhe Mariam Ditopile akikabidhi mifuko ya Saruji aliyoitoa kwa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi UVCCM mkoani Ruvuma kwa ajili ya ujenzi wa Kitega Uchumi cha Umoja huo.
 Mifuko ya Saruji yenye thamani ya Shilingi Milioni Moja na Laki Sita iliyotolewa na Mh Mariam Ditopile kwa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi UVCCM mkoani Ruvuma kwa ajili ya ujenzi wa Hosteli ambayo itatumika kama kitega uchumi cha Umoja huo.
Sehemu ya Wanachama na Wapenzi wa Chama cha Mapinduzi waliohudhuria shamrashamra hizo za Ruvuma ya Kijani zilizoandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi UVCCM ambapo Mbunge wa Viti Maalum, Mhe Mariam Ditopile alitoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Hostel


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini