Na Woinde Shizza Michuzi Tv,Arusha
MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali, (NGO) zimemuangukia Rais Dk.John Magufuli zikimtaka asisaini mabadiliko ya sheria ya uendeshaji mashirika hayo na makampuni yasiyotengeneza faida na taasisi zinazosimamiwa na wadhamini uliopitishwa na Bunge hivi karibuni kwani una mapungufu mengi.
Aidha, wamedai akiusaini ukawa sheria madhara hayatakuwa kwa mashirika hayo pekee bali itawaumiza wananchi wengi ambao hupatiwa huduma na mashirika hayo.
Pia sheria hiyo itaziathiri taasisi mbalimbali za kimataifa na za kikanda zinazoendesha shughuli zake hapa nchini jambo ambalo wameahidi kufikisha suala uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC) na kwa Spika wa bunge la Afrika Mashariki , (EALA ).
Waliyasema hayo jijini hapa walipokutana kwa ajili ya kujadili sheria hiyo ambayo hawakupata fursa ya kuijadili kwani ilipelekwa bungeni kwa hati ya dharura.
Akichangia kwenye mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Madini Amani Mhinda amesema sheria hiyo ikitumika kama ilivyopitishwa na bunge itaathiri wananchi wengi.
"Kwa bahati mbaya haijagusa NGOs peke yake imezigusa na taasisi nyingine ambazo zimesajiliwa chini ya sheria mbalimbali, society act, company act na trustee act ambapo zote zimejumuishwa chini ya NGOs kwa bahati mbaya," amesema Mhinda ambaye pia ni Mwanasheria wa haki za binadamu.
Amesema sheria hiyo itazilazimu taasisi zanazofamya kazi za kusaidia jamii ambazo hazitengenezi faida zilizosajiliwa kama makampuni na chini ya bodi ya wadhamini watatakiwa ndani ya miezi miwili wawe wamejisajili kwa msajili wa NGOs.
"Kuna umuhimu kupewa muda kutafakari athari kabla Rais hajasaini na tunaomba tupate fursa kuendelea na mazungumzo haya kuona sheria ambazo zinakinzana na hali ilivyo," amesema Mhinda na kuongeza.
"Tunafahamu kulikuwa na udhaifu uliopaswa kurekebishwa lakini unaweza kusababisha madhara mengine ya kisheria na kusababisha mashirika mengi kufungwa na kuathiri wananchi waliokuwa wakipatiwa huduma na mashirika haya.
"Kuna wengine walikuwa anafadhiliwa kutoa elimu, elimu na huduma ya afya na pia wanapata tiba kupitia NGO na kwa muda ambao yamefanyika mabadiliko haya haijatoa fursa kwa watu wote kusikilizwa."
Kwa upende wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Civic and Legal Aid, (CILAO), Odero Odero amesema kuwa waathirika wakubwa wa sheria hiyo ni wanufaika wa huduma zinazotolewa na asasi hizo za kiraia hivyo Rais akiisaini na kuanzz kutumia itaathiri shughuli wanazoendelea kufanywa kwa sasa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo,
" Endapo mashirika hayo yatakoma kufanya kazi, wananchi ndiyo watakaoumia zaidi. Hivyo naamini Serikali iko kwa ajili ya wananchi, itatusikia na itatoa muda zaidi wa majadiliano. Tukikaa pamoja tunaweza kujadili kuondoa changamoto zinazoweza kusababishwa na sheria hiyo endapo Rais ataisaini kuanza kutumika," amesema Odero.
Wakati huo huo Mtendaji Mkuu wa chama cha wanasheria wa Afrika, Donald Deya, ambaye ofisi zao ziko jijini Arusha amesema sheria hiyo inaathari kuwa kwa taasisi za kimataifa zilizosajiliwa hapa nchini hivyo akasema kuwa bado uko mlango wa kuipinga sheria hiyo mahakamani.
Aidha ameshauri ni vema suala hilo likapelekwa kwa uongozi wa EAC kwani taasisi nyingi za ukanda huo zimesajiliwa Tanzania na zimeweka ofisi zake Arusha yalipo makao makuu ya jumuiya hiyo.
Mtendaji mkuu wa chama cha wanasheria wa Afrika, Donald Deya
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments