Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Michezo Nchini, Addo Komba amezindua rasmi mashindano ya Mpira wa Miguu na Mpira wa Pete ya Buchimwe Cup 2019 yaliyoandaliwa na Diwani wa Kata ya Buigiri (CCM) wilaya ya Chamwino.
Mashindano hayo yanashirikisha Timu nane Kwa kila mchezo ambapo mshindi wa kwanza atajinyakulia Kombe, Seti Moja ya Jezi na kiasi cha Sh 100,000 taslimu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo Komba amesema Serikali kupitia Wizara ya Michezo itaendelea kuunga mkono maendeleo ya Michezo kwani wanaamini licha ya Michezo kuwa ni Afya lakini siku hizi imekua ni Ajira ambayo imenufaisha kundi kubwa la vijana.
" Nimpongeze Diwani wenu, Mhe Yindi kwa kuandaa mashindano haya, kila mwaka amekua akianzisha Ligi mbalimbali kwa ajili yenu, hii ni faida kwenu na myatumie mashindano haya kukuza vipaji venu na kuhakikisha mnapiga hatua nyingine ya kupata Timu zinashoriki Ligi kubwa," amesema Komba.
Nae Diwani wa Kata hiyo Mhe Yindi amesema pamoja na kuanzisha mashindano hayo pia kutakua na kozi za uamuzi kwa vijana waliomaliza kidato cha nne ambazo zitaendeshwa na wakufunzi kutoka Chama Cha Soka Mkoa wa Dodoma, (DOREFA).
" Lengo la mashindano haya ni kuhakikisha vijana wetu wanapiga hatua, lakini pia kuunga mkono juhudi za Mhe Rais Dk John Magufuli kukuza sekta ya Michezo nchini, na sisi kama watu tunaomsaidia inatubidi kumuunga mkono kwa vitendo.
" Tunafahamu kuwa mna changamoto ya viwanja vya kuchezea, nimeshaanza kushughulikia na nina hakika kupitia Wizara ya Michezo tutamaliza changamoto hiyo," amesema Mhe Yindi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chinonwa, Mhe Joel Mwaka amempongeza Diwani Yindi kwa kuandaa mashindano hayo na kuahidi kutoa mchango wake wa hali na mali katika kila hatua ya mashindano hayo.
Nao wananchi wa Kata hiyo wamemshukuru Diwani huyo kwa kudhamini upatikanaji wa Jezi na Mipira kwa kila timu zinazoshiriki Ligi hiyo kwani kumeongeza ari ya kufanya vema.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments