TIC YAHAMASISHA WAWEKEZAJI KUANZISHA MIRADI YA UWEKEZAJI INAYOLENGA KUONGEZA THAMANI YA MAZAO YA KILIMO | ZamotoHabari.

KITUO cha Uwekezaji Tanzania(TIC) kinawahamasisha wawekezaji wazawa na wageni kuanzisha miradi ya uwekezaji inayolenga kuongeza thamani  mazao ya kilimo ili kuzalisha bidhaa kama vile juice, mvinyo, mafuta ya kula, unga, dawa, maziwa, chakula cha mifugo, samaki na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na mifugo.

Kimesema hayo leo kwenye Maonesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) yanayofanyika  kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam yaliyoanza  Juni 28 Juni, 2019.

Maofisa wa TIC waliokuwa kwenye maonesho hayo wamesema kauli mbiu ya maonesho ni "usindikaji wa mazao ya biashara kwa maendeleo endelevu ya biashara" na kwamba  kauli mbiu hiyo imelenga kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Mhe. Dkt. John Magufuli inayohimiza uanzishaji wa viwanda vya usindikaji.

Wamefafanua kuwa lengo likiwa kuwezesha uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali  zilizoongezwa thamani badala ya kusafirisha malighafi.

 "Lengo ni kuhakikisha  wananchi na Taifa kwa ujumla linanufaika na faida zinazotokana na uwekezaji kwenye mnyororo mzima wa thamani katika sekta ya Kilimo unaohusisha kilimo, usindikaji na biashara kiujumla,"amesema mmoja wa maofisa hao.

Hivyo ili kuunga mkono miradi ya wawekezaji itakayoanzishwa, Serikali inatoa vivutio vya uwekezaji vya  kodi na visivyo vya kikodi kwenye mitambo, mashine na bidhaa nyingine za mtaji zinazohusiana na    mradi. Bidhaa hizo ni zile zinazoagozwa kutoka nje ya nchi.Hata hivyo Wadau  wazingatie kwamba vivutio vya uwekezaji  hutolewa tu kwa miradi iliyosajiliwa na TIC. Lengo ni kusaidia   miradi ya uwekezaji  katika hatua za awali za utekelezaji.

Kwa kujibu wa TIC ni kwamba inawakumbusha wadau  kwamba TIC wanasajili miradi ya uwekezaji inayomilikiwa na wazawa ikiwa na  thamani ya dola za Kimarekani laki moja (100,000) na dola za  Kimarekanilaki tano (500,000) kwa mradi utakaomilikiwa na mgeni au ubia.  Kiasi hicho  pia kinaweza kuwa fedha za Kitanzania zinazolingana na kiasi hicho.

"Kipekee kabisa TIC inawakaribisha wadau (mtu binafsi,kampuni, vyama vya maendeleo na taasisi mbalimbali) kutembelea banda letu ili kupata elimu ya uwekezaji na namna ambavyo wanaweza kunufaika na huduma zetu.  Banda lipo  kwenye hema  la  Jakaya Kikwete (JK),"imesema TIC.
 Ofisa wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Benson Nkini akiweka moja ya bango kwenye banda la kituo hicho lililopo kwenye maonesho ya biashara Sabasaba jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya wananchi wakiwa katika banda la TIC wakipata maelezo kuhusu majukumu ya kituo hicho na hasa katika uwekezaji 
Ofisa wa Huduma kwa Wawekezaji Privata Chiwalo akitoa maelezo kwa wageni waliotembelea banda la TIC


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini