Bolt yazidi kutanua huduma zake katika miji mikubwa Tanzania | ZamotoHabari.


  KAMPUNI inayokua kwa kasi katika utoaji wa huduma za usafiri kwa njia ya mtandaoni barani Ulaya na Afrika- BOLT, inatarajia kuzindua huduma zake katika miji mikubwa miwili nchini Tanzania ikiwa ni hatua mojawapo ya kuendelea kupanua huduma za usafiri katika soko lake la ndani ya nchi.

Huduma hiyo imeanza kupatikana jana Septemba 4, 2019 katika jiji la Arusha na kuanzia wiki ijayo itaanza kupatikana Visiwani Zanzibar.

Uzinduzi huo wa Bolt katika jiji la Arusha na Visiwani Zanzibar unaongeza idadi ya miji ya Kitanzania inayohudumiwa na kampuni hiyo kutoka mikoa mitatu hadi mitano, na kuifanya Bolt kuwa mtoaji huduma mkubwa wa usafiri kwa njia ya mtandao katika ukanda huu wa Afrika.

Meneja wa Bolt Tanzania, Remmy Eseka alisema kuwa dhamira ya Bolt ni kufanya usafirishaji wa mijini kuwa rahisi zaidi na wa bei nafuu kwa watu wote na hivyo kufikia malengo ya kampuni katika utoaji huduma za usafiri na ajira ikiwa ni moja ya mchango Bolt kwa jamii.

"Baada ya miji ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma kama ilivyo ada Bolt imeendelea kukua kwa kasi nchini kote. Sasa tunakusudia kujenga jamii mpya Arusha na Zanzibar kutokana na uaminifu tunaoendelea kuupata kwa Watanzania," alisema Eseka.

Alisema huduma hiyo ni rahisi kutumi kwani abiria wanatakiwa kupakua programu ya Bolt kutoka kwenye maduka ya programu ya iOS au ya Android na kujaza wasifu wa mtumiaji. Wakati wapo tayari kusafiri, watumiaji hufungua program na kuweka eneo lao walilopo na mahali walipokusudia kufika.

Pia Programu itatoa makisio ya gharama kwa safari hiyo.

"Mara baada ya abiria kuomba safari, programu humwonesha madereva wa karibu ambao wanakubali safari hiyo.Mara tu dereva anapokubali safari hiyo, abiria wataweza kuona jina la dereva wao, picha, muundo wa gari na usajili, na kuweza kufuatilia dereva anayewafuata kwa wakati muafaka na wa kweli lakini pia program hiyo hufanya iwe rahisi kuwa na uhakika kuwa wanaingia salama kwenye gari sahihi na dereva sahihi.

"Abiria pia wanaweza kutoa maelezo ya safari yao kwa kutumia program ‘ETA’ iliyomo katika kipengele cha ziada kwenye suala la usalama.

"Wakati safari imekamilika, malipo hufanywa na pesa taslimu, au kupitia kadi ya deni ya mpandaji aliyejiunga kwenye program hiyo. Abiria na madereva wanaweza kupima kila mmoja kati ya nyota tano na kutoa maoni kuhusu umahiri wa utumiaji programu ya Bol," alisema.

Aidha, alisema Bolt tayari imewasajili madereva katika miji ya Arusha na Visiwani Zanzibar, ambao wote wanapokea asilimia 80 ya nauli zote zinazolipwa na abiria.Hata hivyo, madereva wanaotumia Bolt wanaweza kuchagua masaa mangapi wanaendesha na wanaweza kufanya kazi katika maeneo yoyote wanayotaka.

"Magari ya Madereva lazima yawe yamesajiliwa kuanzia mwaka 2000 au mapya zaidi. Gari lazima iwe na milango minne (Toyota Corolla, aina ya Hyundai, Kia Rio, nk). Hii inamaanisha kuwa kila mtu akipanda safari kupitia Bolt anaweza kuwa na hakika kwamba watafika salama kwao na kwa raha," alisema.
Mwisho


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini