BEI ya mafuta imepanda kwa kiwango cha juu kuwahi kushuhudiwa katika miezi minne baada ya mashambulio mawili dhidi ya vituo vya mafuta Saudi Arabia, juzi, Jumamosi yaliyosababisha kumwagika (kupotea) kwa asilimia 5 ya mafuta duniani.
Kiwango cha mafuta ghafi kilipanda kwa asilimia 19 kwa thamani ya Dola 71.95 kila pipa huku viwango vingine, West Texas Intermediate, vikipanda kwa asilimia 15 kwa thamani ya Dola 63.34. Bei zilishuka kidogo baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuagiza kufunguliwa kwa akiba nchini Marekani.
Huenda ikachukua wiki kadhaa kabla ya vituo hivyo Saudia kurudi katika hali ya kawaida. Kampuni kubwa ya mafuta ya Saudia Aramco imesema mashambulio hayo yalikatiza usambazaji kwa mapipa milioni 5.7 kwa siku.
Mashambulio hayo dhidi ya vinu katika shina la viwanda vya mafuta nchini Saudia vinajumuisha kituo kikubwa duniani cha usafishaji mafuta.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, amesema Tehran (Iran) imehusika na mashambulio hayo. Iran imeishutumu Marekani kwa ‘uongo’.
Baadaye Trump amesema katika ujumbe wa Twitter kuwa Marekani inafahamu mhusika wa uhalifu huo ni nani na ipo tayari ila inasubiri kusikia kauli ya Wasaudia kuhusu namna ambavyo inataka kulifuatilia suala hili.
Wasaudia hawajaeleza kwa kina kuhusu mashambulio hayo, mbali na kusema kwamba hakuna aliyeathirika, lakini imetoa ishara kidogo kuhusu uzalishaji wa mafuta.
Waziri wa Nishati, Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman, amesema kupungua kwa uzalishaji mafuta kutafidiwa kwa kutumia akiba kubwa iliyopo.
Ufalme huo ndio wauzaji wakuu wa mafuta duniani, ambapo unasafirisha zaidi ya mapipa milioni saba kwa siku ya mafuta.
“Maafisa wa Saudia wamedai kudhibiti moto huo, lakini si kuwa umezimwa kikamilifu,” amesema Abhishek Kumar, mkuu wa takwimu katika shirika la Interfax Energy mjini London na kuongeza:
“Uharibifu kwa vituo vya Abqaiq na Khurais unaonekana kuwa mkubwa, na huenda ikachukua wiki kadhaa kabla ya usambazaji mafuta kurudi katika hali ya kawaida.”
Saudi Arabia inatarajiwa kutumia akiba iliyopo ili usafirishaji mafuta uendelee kama kawaida wiki hii.
Iran imeishutumua Marekani kwa ‘uongo’ na waziri wake wa mambo ya nje, Javad Zarif, amesema kuwa “kuituhumu Iran hakutomaliza janga” nchini Yemen.
Yemen imekumbwana vita tangu 2015 wakati Rais Abdrabbuh Mansour Hadi alipolazimishwa na waasi wa Houthi kuukimbia mji mkuu Sanaa.
Saudi Arabia inamuunga mkono Hadi, na inaongoza muungano wa mataifa ya eneo hilo dhidi ya waasi hao.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA
0 Comments