Ndugu zangu,
Nimeangalia picha za video na mnato kuhusu kinachoendelea Afrika Kusini.
Xenophobia, ni hali ya wenyeji kujiona wana haki zaidi na kuwakataa wageni katika jamii. Huu ni ugonjwa, tunao umetuganda.
Tatizo lipo, tena kubwa na linahitaji tiba ya haraka. Ni namna tu ya kuliendea tatizo hilo. Hata sisi katika mikoa yetu tunazo chembe za Xenophobia ila pengine aina ya maamuzi tunayochukua ndiyo hayafanani.
Nakumbuka nikiwa mdogo mkoani Tanga, wakubwa zetu walitujengea mazingira ya kuwachukia Wasambaa. Kabila hili linatokea milimani Wilaya ya Lushoto.
Tulikuwa tunawachukia bila sababu, tuliwapa majina mabaya. Kila lisilofaa au kila tabia isiyofaa ilinasibishwa na kabila la wasambaa.
Walionekana watu wa hovyo, walionekana wana vurugu na kila baya. Wachafu, hawana staha na mengi ambayo naona haya hata kuyataja hapa
Sababu ya hayo ni uvivu wa kaka na pengine baba zetu, hawakutaka kazi ngumu kama kubeba mizigo sokoni, kuuza mihogo na kutembeza kahawa barabarani.
Wasambaa walifanya kila kazi; mradi hawakuvunja sheria. Mbali ya kudharauliwa hawakuvunjika moyo.
Hivi nizungumzapo asilimia kubwa ya wale vijana wa Kisambaa ambao ni mahamia wa Tanga katika mika ya 1970 na 1980 hadi 1990 leo ndio matajiri wa Tanga.
Wanamiliki maduka, mabasi na biashara ya nafaka. Wanamiliki asilimia 80 ya biashara katika soko kuu la Ngamiani. Wana fedha.
Sisi watoto wa 'Kiungwana' tuliowabeza tumeishia kusubiri 'maa' (Mama) au 'baa' (Baba) atoe pesa ndio nyumbani kuliwe.
Sisemi vijana wote wa Tanga mjini hawataki kazi, la. Ila wapo waliojiendeleza kwq elimu, kazi za ajira au biashara.
Hiki ndicho kinachotokea sasa Afrika Kusini. Baada ya uhuru mwaka 1994, wenyeji walidhani zile nyumba, magari, mashamba na biashara walizokuwa wakishikilia Makaburu watapewa wao; bure.
Nelson Mandela, akawaambia hawa Makaburu hapa ndio kwao. Hawana pa kwenda kwani walifika 'Cape of good hope' mwaka 1488.
Historia inasema mzungu wa kwanza kufika Caoe Town ni Mreno, Bartolomeu Dias mwaka huo wa 1488.
Baadaye mwaka 1497 Mdachi, Vasco da Gama alipita wakati akiitafuta India. Alikaa bandari ya St. Helena Bay kwa siku nane ndipo akavutiwa na mandhari ya Afrika Kusini.
Aidha, kampuni ya kwanza ya Kidachi ambao ndio asili ya Makaburu, ilianza biashara mwaka 1647. Ikiitwa The Dutch East India Company.
Sasa Mandela aliuliza watu hao unawaambia warudi kwao baada ya kukaa katika ardhi hiyo kwa miaka zaidi ya 400.
Hilo liliwavunja nguvu, wengi hawajui kama Mandela si maarufu na hapendwi sana Afrika Kusini kuliko nchi nyingine za Afrika. Sababu ni hiyo, anaonekana 'Snitch.'
Kuanzia miaka ya 1995 waafrika kutoka kila kona ya bara hili wakaanza kumiminika kutafuta fursa. Kutoka Tanzania, Zimbabwe, Nigeria, Kenya na kwengine kwingi.
Mwanzo raia wa Afrika Kusini waliona kawaida, ila kadiri siku zilivyokwenda mambo yakawawia magumu.
Raia wa kigeni hawana makuu, wakipanga nyumba ya vyumba vitano watakaa hata 50. Wakila mlo mmoja poa, wakikosa wanashukuru. Hivyo, ajira ya mshahara wowote kwake ni neema.
Wenye akili walifanya kazi kama mbwa bata kazi nne kwa siku. Kila wakilipwa wanatuma pesa kwao kujenga nyumba, kusomesha ndugu zao na kulea familia.
Sasa mambo yamegeuka. Raia wanataka kurudishiwa kazi zao. Wameshacheleqa maana serikali haina cha kuwapa. Na matajiri ambao asilimia kubwa ni wahindi na wazungu wameshazoea waahiriwa wanaotaka mshahara mdono na wanaofanya kazi kubwa.
Raia wao wanataka kazi na bata.
Makala hii kwa hisani ya Mhariri wa Jamvi la Habari-Hafidhi Kido
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments