MVUA ZA VULI ZITAKUWA ZA WASTANI -MAMLAKA YA HALI YA HEWA. | ZamotoHabari.

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV.

MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imesema kuwa, mvua za vuli zinazotarajia kuanza kunyesha kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba 2019 zitakuwa za wastani hadi chini ya wastani.

Mvua hizo zinatarajiwa kunyesha katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na Pwani ya Kaskazini.Huku Mikoa ya Kanda ya Ziwa Viktoria pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma mvua zinatarajia kunyesha za wastani hadi juu ya wastani.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi amesema hayo leo Septemba 3, 2019 jijini Dar es Salaam, wakati akitoa utabiri wa Hali ya Hewa msimu wa mvua za vuli ambazo hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Nyanda za juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.

Dkt. Kijazi amesema, joto la juu ya wastani katika bahari ya Hindi linatarajiwa kuongezeka katika kipindi hicho huku uwezekano wa matukio ya vimbunga katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi yanaweza kutokea.

Ameongeza kuwa kwa mikoa mingi mvua hizo zinatarajia kuanza kunyesha katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba na kumalizika wiki ya nne ya mwezi Desemba 2019 katika baadhi ya maeneo

Amesema, mvua za nje ya misimu zinazoendelea kunyesha mkoani Kagera toka mwezi Agosti na zinatarajiwa kuendelea kunyeshaa hadi kufikia wiki ya pili ya mwezi Oktoba na hivyo zitaungana na msimu wa mvua za vuli ambazo zinatarajiwa kumalizika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Januari 2020.

"Mvua hizo zinatarajiwa kuendelea kusambaa katika Mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Simiyu na Shinyanga katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba. Kiwango cha mvua kinachotarajiwa katika msimu huu ni mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda huo," amesema Dkt.Kijazi 

Amesema mvua katika ukanda wa Pwani ya Kaskazini katika mikoa ya Dar es salaam,Tanga,Pwani,Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro zinatarajiwa kuanza kunyesha katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba ingawa mtawanyiko wake unatarajiwa kuwa hafifu.

Pia kutakuwepo vipindi virefu vya ukavu na mvua chache zinatarajiwa kuwepo katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini ambapo kutakuwa na mvua za wastani kuanzia wiki ya pili ya mwezi Novemba na kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Disemba.

"Katika mikoa ya Nyanda za juu Kaskazini Mashariki Mikoa ya Kilimanjaro,Arusha na Manyara mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Oktoba kutarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa hiyo ambapo Mvua hizi zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Desemba 2019," amesema Dkt Kijazi

Dkt. Kijazi amesema, katika maeneo yanayotarajiwa kuwa na mvua nyingi matukio ya magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza na pia maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani pia yanaweza kupata magonjwa ya mlipuko kutokana na uhaba wa Maji safi na salama

"Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinarajiwa kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani na chini ya wastani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Dk. Agnes Kijazi akitangaza utabiri wa msimu wa mvua za vuli kwa waandishi wa habari katika kipindi, cha Octoba hadi Disemba, 2019 (OND). Utabiri huo umetangazwa leo Septemba 3, 2019 kwenye makao makuu ya Mamlaka ya Hali ya hewa (TMA) Ubungo Plaza jijini Dar es salaam kulia kwake ni Mkurugenzi wa Huduma za utabiri, Hamza Kabelwa, na kushoto ni Meneja wa huduma za utabiri Samwel Mbuya.
baadhi ya wanahabari na wadau wa TMA wakifuatilia utabiri huo


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini