Mfungaji tegemeo wa TAMISEMI QUEENS Lilian Jovin akifunga mojawapo ya magoli muhyaliyoiwezesha timu yake kushika nafasdi ya pili katika michuano ya netiboli ligi daraja la kwanza inayoendelea katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma
……………………
Na Mathew Kwembe, Dodoma
Timu ya netiboli ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ‘TAMISEMI QUEENS’ imejigamba kufanya vizuri katika michuano inayoendelea ya netiboli ligi daraja la kwanza inayoendelea katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Tayari timu hiyo imeshinda michezo minne kati ya sita iliyokwishacheza na hivi sasa inashika nafasi ya pili mbele ya vinara timu ya Mbweni JKT kutoka jijini Dar es salaam.
TAMISEMI QUEENS imekwishazifunga timu za Cocacola,Jiji la Dodoma, Jiji la Tanga na SMART na imepoteza michezo miwili hadi sasa ambayo ni ya Mbweni JKT na Jiji la Arusha.
Akizungumzia michuano hiyo kocha wa timu hiyo Maimuna Kitete amesema kuwa timu yake ina nafasi nzuri ya kushiriki ligi ya muungano kutokana na maandalizi mazuri ambayo timu yake imeyafanya.
Amesema kufikia sasa timu yake imeonyesha upinzani mzuri dhidi ya timu tishio kama Mbweni JKT na ameahidi kuzichapa timu zote tatu zilizosalia katika michuano hiyo.
Kwa upande wake Meneja wa timu hiyo Doto Bintaraba amesema kuwa timu ya ‘TAMISEMI QUEENS’ ina uhakika wa kushika nafasi tatu za juu kutokana na kuwaandaa vijana wake kufanya makubwa katika michuano ya ligi daraja la kwanza inayoendelea jijini Dodoma.
Amesema ari kubwa waliyo nayo wachezaji wake imempa imani ya kuendelea kufanya vizuri katika mechi tatu zilizosalia.
Naye mchezaji Lilian Jovin ambaye ndiye mfungaji tegemeo wa ‘TAMISEMI QUEENS’ amesema kuwa timu yake inaendelea kuimarika siku hadi siku na akaahidi kufanya vizuri katika michuano iliyobaki ya ligi daraja la kwanza.
Amesema kuwa kufikia sasa timu yake haiwaogopi timu yoyote na akawatahadharisha timu pinzani watakazokutana nazo wajipange kupata kipigo kitakatifu.
Kauli ya Lilian iliungwa mkono na mchezaji mkongwe wa timu hiyo Flora Odilo ambaye aliahidi ushindi mnono kwenye michezo mitatu iliyosalia katika michuano ya ligi hiyo.
‘TAMISEMI QUEENS’ imebakiza mechi dhidi ya Eagle, JKT Makutupora na JKT Mbweni.
Hadi sasa wanaoongoza ligi hiyo ni timu ya JKT Mbweni yenye pointi 10, ikifuatiwa na ‘TAMISEMI QUEENS’ikiwa na pointi 8, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na timu ya JKT Makutupora iliyo na pointi 8 pia huku nafasi ya nne na ya tano zikichukuliwa na timu za Jeshi Stars na Jiji la Arusha.
Mbali na michuano hiyo kutoa bingwa wa mchezo wa netiboli Tanzania Bara, timu sita za juu zitafanikiwa moja kwa moja kushiriki ligi ya netiboli ya muungano iliyopangwa kufanyika mjini Zanzibar baadaye mwaka huu.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments