Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Harrson Mwakyembe akizungumza na wadau wa soka katika uzinduzi wa tamasha la Kahama United Sport Academy
Na Mwandishi Wetu, Kahama
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo imewataka Watanzania na wawekezaji kutoka nje ya nchi kuwekeza katika kujenga maduka makubwa ya vifaa vya michezo na viwanda ili kupunguza gharama za kuagiza kutoka nchi za nje.
Kwa sasa Serikali ipo katika mazungumzo na baadhi ya wawekezaji kwa ajili ya kuona umuhimu wa kujenga viwanda na maduka makubwa ya vifaa vya michezo ili wananchi wanunue kwa bei ndogo na hatimaye kukuza sekta ya michezo nchini Tanzania ambayo ina nafasi kubwa ya kutoa ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi katika taifa.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dk.Harison Mwakyembe aliyasema hayo wakati akizindua Kituo cha kulelea watoto cha Kahama United Spots Academy ambapo amesema kwa sasa nchi ipo katika mapinduzi makubwa ya michezo.
Dk.Mwakyembe amesema anawakaribisha watanzania na wawekezaji kutoka nje ya nchi wenye uwezo wa kuwekeza kupitia katika Wizara yake na kuzungumza nao ili kufanikisha upatikanaji wa vifaa vya michezo hapa hapa nchini na hivyo kupunguza bei ya kununua vifaa hivyo.
Aidha amesema Tanzania ipo vizuri katika suala zima la michezo na kuongeza kuwa mradi huo ulioanzishwa na wadau wa soka wilayani Kahama ni mkubwa na kwamba wilaya na mikoa mingine itaiga mfano huo huku akiwapongeza wadau wa michezo Wilaya ya Kahama kwa kuanzisha kituo hicho.
Hata hivyo Waziri Mwakyembe ameutaka uongozi wa Kahama Spots Academy kuhakikisha kuwa inatafuta maeneo makubwa nje ya mji kwa ajili ya uwekezaji wa michezo badala ya kung’ang’ania kuwekeza mijini ambapo maeneo ni madogo.
Awali akisoma risala ya kituo hicho Katibu wa Bodi ya Kahama Spots Academy Shabani Nguno amesema kuwa vijana waliopo katika kitu hicho ni wa umri wa kuanzia miaka 15, 17, pamoja na 20 huku wengi wao wakiwa ni wanafunzi wa shuyle mbalimbali za sekondari katika Wilaya ya Kahama.
Nguno amesema kuwa vijana wote katika kituo hicho wanapata mafunzo ya kuanzia madarasani na katika michezo na kuongeza kuwa watu matajiri kwa sasa wanatokana na michezo na hivyo wameamua kuwekeza ili kuwasaidia vijana hao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kahama Spots Academy Khamis Mgeja amesema lengo kubwa la kituo hicho ni kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli kwa kutumia sekta ya michezo katika kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla na wadau wa kahama wakaamua kujikita kuwekeza katika michezo.
Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya Kahama Anamringi Macha amesema wazazi kuhakikisha kuwa wanawahimiza watoto wao kuwa na utamadumni wa kupenda michezo kwani inasaidia katika kujenga mwili na kukuza akili kwa ujumla wake.
Macha amesema Kahama kuna fursa nyingi na rasilimali za kutosha ikiwa ni pamoja na maeneo makubwa kwa ajili ya viwanja vya mpira na michezo mingine na kuongeza kuwa kwa kufunguliwa kituo hicho ni moja ya matunda ya kukuza michezo kahama.
Katika hafla hiyo Waziri Mwakyembe alizawadiwa na Academy kupitia Mwenyekiti wake Alhaji Abed Salum jezi ya timu yenye jina la Mwakyembe.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments