Waziri Mahiga "Vilivyoibiwa ni Vipande vya Kompyuta Mbili na Ofisi ya DPP Haijaguswa" | ZamotoHabari.


Waziri wa Sheria na Katiba nchini, Dk Augustine Mahiga, amesema vilivyoibiwa ni vipande vya kompyuta na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga,ipo salama haijaguswa.

Kadhalika,nyaraka zote za uhujumu uchumi ziko salama na ofisi ya DPP hakuna kilichoibiwa.

Mahiga aliayasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa kompyuta zilizoibiwa ni ofisi ya Mashtaka mkoa wa Dar es Salaam na sio ofisi ya DPP.

“Vyombo vya habari mmetoa taarifa, kwa mfano gazeti la leo limesema, nyaraka muhimu zinazohusiana na watuhumiwa walioko mahakamani zimeibiwa na zimesababisha kesi hizo kuathiriwa,” amesema bila kutaja gazeti hilo

“Ukweli ni kwamba, ofisi ambayo ilivunjwa na baadhi za kompyuta, si zote bali ni vipande tu. Ofisi ya Mkurugenzi mkuu wa mashitaka ya serikali haikuguswa, nyaraka zote zipo, taarifa zote zipo na kazi yake inaendelea,” amesema Waziri Mahiga

Waziri alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza uhalifu huo ili hatua zichukuliwe.

“Hivyo vipande vya kompyuta ni sehemu ya vizibiti ambavyo polisi wanachunguza. Nataka kuwahakikishieni kwamba ofisi ya DPP haijaathiriwa hata kidogo” alisema

Alisema ofisi hiyo ya mkoa haikuwa na nyaraka za uhujumu uchumi bali inahusika na ukusanyaji wa taarifa ambazo hata hivyo hakuzitaja.

“Kwanza ni ofisi ndogo ambayo haina nyaraka, bali ni ukusanyaji wa taarifa tu iko hapo Mkwepu street na sio kompyuta zote ni vipande vya kompyuta mbili.”

” Lakini taarifa zote zinazohusu uhujumu uchumi zipo kwa DPP na ofisi yake haikuguswa na shughuli zake zitaendelea ambazo ametumwa. Kazi inavyoendelea DPP itabidi apeleke taarifa kwa Rais halafu tujue tunakwendaje,” amesema

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini