DOGO aliyepata umaarufu mkubwa kupitia ushiriki wake kwenye Shindano la Kusaka Vipaji la Bongo Star Search (BSS) 2019, Hamisi Saidi, amekana kusainiwa kwenye Lebo ya Konde Music Worldwide ya mwanamuziki wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ au ‘Harmo’.
Katika shindano hilo lililofikia tamati usiku wa Mkesha wa Krismasi, mwaka huu, dogo huyo ambaye ni maarufu kwa jina la Hamisi BSS aliishia Tano Bora ambapo Meshack Fukuta wa Mbeya ndiye aliibuka kidedea. Kwa upande wake, Hamisi BSS kumekuwa na stori nyingi mitandaoni juu ya yeye kuchukuliwa na Harmo, lakini mwenyewe amemkana jamaa huyo.
Gazeti hili lilitaka kujua mipango yake baada ya kumalizika kwa shindano hilo huku kukiwa na habari za kusainiwa na Harmo ambapo alisema; “Kwa sasa sina timu yoyote, sijawasiliana na Harmonize wala mtu yeyote kunipigia simu kuhusu suala hilo. Sijawasiliana na yeyote.
“Kwa sasa naangalia namna ya kujiendeleza na Mungu akipenda nitarudi tena kwenye BSS mwaka ujao,” alisema Hamisi BSS na kuongeza; “Unajua wakati nikiendelea na mazoezi kwenye BSS nilikuwa siko sawa kiafya. Nilikuwa ninasumbuliwa na tatizo la sauti kwa muda mrefu na hata walimu wangu kwenye mashindano walikuwa wanalijua hilo.
“Najua nina mashabiki wengi sana nyuma yangu na sijui kama kuna BSS itatokea halafu kukawa na mshiriki mwenye mashabiki wengi kama nilivyokuwa mimi, lakini nawaomba radhi pale nilipowaangusha kwani kuna wakati niliona kama wenzangu ni wakali zaidi na ilikuwa lazima mshindi mmoja apatikane, japokuwa sijajua kigezo kinachotumika kumpata mshindi kwani kama ni kura, mimi nilikuwa na kura nyingi kuliko washiriki wote.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA
0 Comments