MENEJA BANDARI ZA ZIWA TANGANYIKA AELEZEA UJENZI WA MIUNDOMBINU KATIKA BANDARI YA KIPILI, KIRANDO | ZamotoHabari.

Muonekano wa bandari ya Kipili baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuboresha miundombinu ya bandari hiyo iliyopo mkoani Rukwa .
 Mfanyabiashara kutoka nchini Congo Moise Labola Kaswela akizungumza kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kuboresha miundombinu ya bandari ambapo ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Dk.John Magufuli kwa hatua anazochukua kuimarisha huduma za bandari
 Muonekano wa  bandari ya Kirando ambayo TPA haijaanza kuiboresha ingawa tayari iko kwenye mkakati wa kuhakikisha nayo inaboreshwa ili iendelee kutumika hasa kwa kuzingatia eneo hilo kuna shughuli nyingi za kibiashara
 Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Percival Salama akizungumzia ujunze wa miundombinu katika bandari za Kipili, Kirando mkoani Rukwa


*Wafanyabishara kutoka nchini Congo watuma ujumbe kwa Rais Magufuli kuhusu ujirani mwema

Na Said Mwishehe, Michuzi Globu - Rukwa

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) imesema kuwa ujenzi wa miundombinu katika bandari ya Kipili upo hatua za mwisho kukamilika ambapo awamu ya kwanza ya ujenzi imegharimu Sh.bilioni 4.356 na mradi wa pili katika bandari hiyo umehusisha ujenzi wa barabara ambapo Sh.milioni 448 zimetumika.

Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Percival Salama amesema katika Mkoa wa Rukwa , TPA imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya bandari zilizoko katika mkoa huo na moja ya bandari ambazo zimepewa kipaumbele ni ya bandari ya Kipili ambapo miundombinu imeboreshwa.

"Katika bandari ya Kipili  mradi wa kwanza ulikuwa wa Sh. bilioni 4. 356 na mradi wa pili ambao umeteleleza ni wa Sh.milioni 448 ambao umehusisha uwekaji wa  barabara ili iwe rahisi kufika kwenye gati vizuri, sehemu ya kupaki magari, eneo la kugeuzia magari na eneo la mizigo kabla ya kupakia kwenye meli.

"Tumeboresha miundombinu na sasa iko vizuri.Eneo la pili katika Mkoa wa Rukwa  tunatarajia kufanya uboreshaji katika bandati ya Kirando ambako kuna shughuli nyingi za kibiashara kati ya upande wetu wa Tanzania na wenzetu wa nchi jirani ikiwemo ya Congo,"amesema Salama na kusisitiza kuwa TPA kwa niaba ya Serikali inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli imeweka mikakati ya kuhakikisha huduma za bandari zinakuwa bora na hivyo moja ya kazi inayoendelea ni kuboresha miundombinu ya bandari hizo.

Wakati huo huo wafanyabishara kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo wamempongeza Rais Dk.John Magufuli kwa anachukua za kuboresha miundombinu ya bandari zilizopo Ziwa Tanganyika ambapo wamesisitiza  kuwa hatua hizo zinaleta matumaini makubwa kwao hasa kwa kuzingatia wamekuwa wakija nchini Tanzania kuchukua bidhaa za aina mbalimbali kwa ajili ya kwenda kuuza nchini kwao.

Akizungumza na Michuzi Globu ya jamii akiwa katika bandari ya Kirando iliyopo Ziwa Tanganyika, mfanyabishara kutoka Congo Moise Labola Kaswela amesema Rais Magufuli anafanya kazi kubwa na nzuri na wao wafanyabishara wa Congo wanaiona na hivyo wanampongeza hasa kwa namna anavyoboresha miundombinu ya bandari ikiwemo ya Kapili ambayo ujenzi wa miundombinu umekuwa ukiendelea kwa kasi ya kuridhisha na kwa upande wa gati tayari imekamilika.

"Wafanyabishara wa Congo ambao tunakuja huku Tanzania kila siku kufuata bidhaa mbalimbali kwa kutumia Ziwa Tanganyika, tunampongeza Rais Magufuli, ikitokea siku tukamuona tutamueleza furaha ambayo tunayo.Hata hivyo tutamuomba aendeleze ujirani mwema kwa kutusaidia kutuweke mazingira mazuri zaidi ya kufanya biashara, nikiri mazingira ya biashara ya Tanzania ni mazuri na ndio maana  wafanyabishara kutoka Congo wengi tunakuja kuchukua bidhaa lakini ombi letu kwa Rais Magufuli atusaidie kuimarisha ujirani mwema ambao utatuwezesha kufanyabiashara vizuri zaidi ya sasa,"amesema Kaswela.

Amesisitiza Serikali ya Tanzania inajitahidi katika kuboresha miundombinu , hivyo na wao wataendelea kutumia fursa ya uzuri wa miundombinu hiyo ya bandari kuimarisha biashara baina ya pande hizo mbili huku akisisitiza umuhimu wa bandari nayo kuwekewa miundombinu mizuri kama bandari ya Kipili.

Kwa upande wake Mkazi wa Kirando ambaye anajishughulisha na biashara katika Bandari ya Kirando Seif Kassim Seba amesema kwa sasa miundombinu ya bandari ya Kipili imeimarishwa na hivyo wamekuwa na matumaini ya kuongeza kasi ya biashara kati ya Tanzania na Congo.

" Miundombinu ya bandari ikiboreshwa itasaidia kuvuta wafanyabiashara.Kwa hapa Kirando tunahitaji jengo la kupumzika abiria, jengo la vyoo pamoja na miundombinu mingine muhimu.Hata hivyo lazima tukiri kazi ya uboreshwaji wa miundombinu ya bandari zetu katika Ziwa Tanganyika tunaiona,"amesema.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini