Profesa Kabudi: Uhusiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia ni imara na unaendelea vizuri, Yapuuzeni Hayo Yanayosemwa Mitandaoni | ZamotoHabari.




Benki ya Dunia imesema mahusiano na baina ya Serikali ya Tanzania na benki hiyo ni imara na kuihakikishia Tanzania ushirikiano madhubuti katika sekta mbalimbali za kimaendeleo.

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bi. Mara Marwick amesema hayo katika ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianomwa Afrika Mashariki, jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb).

 Bi. Marwick amesema uhususiano baina ya benki hiyo na Tanzania ni mzuri na kwamba Benki ya Dunia inathamini uhusiano huo wa tangu miaka ya 1960 hadi leo na iko tayari kuendelea kuunga mkono kwa njia ya ufadhili au mikopo miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

"Tuna uhusiano mzuri katika miradi na uwekezaji ambapo tunaiwezesha serikali katika maeneo mbalimbali. Pia tunafanya kazi pamoja katika masuala muhimu kama vile uchambuzi wa sera za maendeleo hii inaashiria kuwa Benki ya Dunia itaendeleza ushirikiano huu katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na mahusiano imara pamoja na maendeleo endelevu," Amesema Bi. Marwick.

Ameongeza kuwa katika mazungumzo hayo, wamejadili masuala muhimu kuhusu maendeleo ya Tanzania hususani elimu, miradi ya miundombinu, uchumi wa viwanda, pamoja na maendeleo ya wananchi. 

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema Tanzania itaendeleza mahusiano na Benki ya Dunia na kuwataka watanzania kupuuza uzushi na uvumi unaosambazwa katika mitandao ya kijamii kuhusu mahusiano baina ya Tanzania na Benki hiyo na badala yake wasubiri taarifa rasmi kutoka kwa Serikali na Benki ya dunia.

"Uhusiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia ni imara na unaendelea vizuri, na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia ametuhakikishia kwamba katika kipindi hiki ambacho yeye ni mkurugenzi hapa atauendeleza uhusiano huo huo. Mengi yanasemwa lakini mengi hayana ukweli na wakati mwingine si busara kwa kila yanayosemwa kuyajibu kwasababu yanaweza kuwaondoa kwenye shughuli za msingi na mkajikuta kila siku mnajibu uvumi au uzushi katika mitandao ya kijamii na mambo mengine," Amesema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa katika mazungumzo hayo pia wamegusia miradi ya kimkakati ambayo Tanzania inaitekeleza, mingine kwa fedha za ndani au kwa kupata mkopo kutoka Benki ya Dunia.

"Tumezungumza kwa kirefu kuhusu mashirikiano katika elimu hasa elimu ya wasichana na kukuza rasilimali watu na kutaja maeneo mengine ya mashirikiano ambayo ni pamoja na  sekta za miundombinu, afya, maji na nishati," Ameongeza Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa Tanzania inakopesheka kwenye benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Afrika Mashariki ya Maendeleo na taasisi nyingi sana za kifedha na daima Serikali huhakikisha kuwa vigezo vyote vinavyotakiwa vinasimamiwa lakini kikubwa hulipa madeni iliyokopa na ndiyo maana inaaminiwa na kukopeshwa zaidi na fedha yote inayokopwa hupelekwa kwenye miradi ya msingi ya kulifanya taifa kujitegemea lenyewe katika miaka michache ijayo.

Katika tukio jingiene, Waziri kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Stegomena Taxi na kujalidiana nae mambo mbalimbali kuhusu SADC.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini