ARUSHA YAZINDUA ZOAEZI LA KUPULIZA DAWA KUUWA VIJIDUDU NA KUWAKINGA ABIRIA NA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA CORONA | ZamotoHabari.


Na Jusline Marco;Arusha

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe.Gabriel Daqarro amezindua zoezi la upulizaji wa dawa ya kuuwa vijidudu kwa lengo la kuwakinga abiria na maambukizi ya virusi vya Corona pindi wanapotumia vyombo vya usafiri.

Zoezi hilo limezinduliwa leo rasmi kwa mabasi yanayotoka Jiji la Arusha kuelekea mikoa mingine , pamoja na vyombo vingine vya usafiri wa umma vinavyotumika katika safari za ndani ya Jiji la Arusha.

Mhe.Gabriel Daqaro amesema kuwa operesheni hiyo ya upulizaji wa dawa utakuwa endelevu na utashirikisha wadau ambao tayari wameanza kutoa michago yao kuwezesha zoezi hilo.

Aidha Daqarro amewataka wananchi kutokuwa na taharuki na hofu pamoja kuzusha maneno ya upotoshaji juu ya ugonjwa huo bali waachie mamlaka husika kutoa taarifa pamoja na elimu.

"Kuna watu wana dhana potofu wanasema Corona haiwezi kuwapata watu weusi hayo ni mawazo potofu kikubwa ni kuchukua tahadhari na kufata maagizo ya wataalamu wetu wa afya" amesema mkuu huyo wa wilaya.

Naye mganga mkuu wa jiji la Arusha Dr. kheri Kyaga amesema kuwa ni vyema wasafirishaji wote wakahakikisha abiria wanatumia vitakasa mikono au kusafisha mikono kwa maji tiririka kabla ya kupanda chombo cha usafiri ili wafike salama bila maambukizi ya ugonjwa huo.

Amesema kuwa maeneo ya stendi yanauwezekano mkubwa wa kuambukizana hivyo jukumu kuu ni kunawa mikono na kuepuka misongamano isiyo ya lazima kwani itasaidia kuepukana na janga hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha usafirishaji mkoa wa Arusha na Kilimanjaro (AKIBOA) Locken Adolf Massawe amesema zoezi la upuliziaji dawa vyombo vya usafirishaji ni endelevu na litahusisha vyombo vya usafiri wa jumuia ambapo bodaboda, magari makubwa na madogo.

" AKIBOA tutaendelea kushirikiana na Serikali katika vita dhidi ya ugonjwa huu"amesema.

Sambamba na mpango huo,Chama cha wasafirishaji abiria (AKIBOA) na wadau wa usafirishaji wametoa vifaa kinga vikiwemo vitakasa mikono pamoja na dawa za kupulizia vyombo vya usafiri vyenye gharama ya Shilingi milioni 7 ili kusaidia wananchi kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Gabriel Daqarro akipuliza dawa ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa corona katika moja ya mabasi kwenye uzinduzi wa zoezi hilo uliofanyika stendi ya mabasi makubwa jijini humo.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini