Askofu asikitishwa na kauli ya Polepole kuwafananisha upinzani na Corona | ZamotoHabari.



Askofu wa Kanisa la Katoliki la Rulenge Wilaya ya Ngara, Severine niwemugizi, amesema amesikitishwa na maneno yaliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole akiwafananisha upinzani na ugonjwa wa virusi vya Corona

“Nimesikitika sana kusoma maneno kwenye mtandao ambayo sijaamini yamesemwa kweli na mtu ambaye huko nyuma nilimheshimu sana, kwamba, tunaomba Mungu ugonjwa huu uondoke, Corona ni sawa na wapinzani nchini“. Askofu aliandika ujumbe huo katika ukurasa wake wa Face book.

Alisema aliyakumbuka maneno ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Anna Mgwira aliyosema kwenye salamu zake baada ya ibada ya kumsimika Askofu Ludovic Joseph Minde kuwa Askofu wa Moshi.

Alisema kwa kurudia rudia „tusaidieni (viongozi wa dini) kuwatengeneza watu wema wanaoheshimu utu wa watu na haki za watu“. Nimejiuliza hivi kweli hiyo ni siasa safi binadamu kumwona au kumuita mwenzake ni sawa na kirusi cha Corona?

“Kumwona binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni tusi kubwa kwa Mungu mwenyewe kwamba yeye Mungu naye ni sawa na kirusi cha Corona, kinachopaswa kuondoka!! Halafu unamwomba huyo Mungu aondoe Corona?!,”

Hapo ndipo tumefika Watanzania kweli!? Hiyo ndiyo sura ya, siasa ni uadui“. Mtu mnayetofautiana mtazamo au itikadi ni adui, ila kesho akibadili mtazamo akafuata wako anabadilika na kuwa lulu nzuri, rafiki, na binadamu kama wewe.

Jamani! Nawasihi Watanzania tujitahidi kupima maneno tunayozungumza hadharani kumhusu binadamu mwingine.

Mtakatifu Yakobo anasema „Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, anaweza kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu“ (Yak 3:2). Na tena, ulimi ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti“ (3:8).

Namshauri aliyesema Corona ni sawa na wapinzani katika nchi hii kama ni muungwana aombe radhi kwa kumdhalilisha Mungu aliyemuumba binadamu kwa sura na mfano wake (Mwa 1:26-27).

Kwa namna hiyo ataepusha mauti kwa heshima yake mwenyewe na kwa siasa za kistaarabu.

APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini