Hakuna Aliye Salama..Mcheza MPIRA wa Juventus Akutwa na Virusi vya Corona | ZamotoHabari.



Juventus imetangaza kwamba beki wa kati wa Italia Daniele Rugani amekutwa na virusi vya corona.

Klabu hiyo ya ligi ya Serie A imesema kwamba imechukua hatua zote za kumtenga mchezaji huyo zinazohitajika kisheria ikiwemo kuwashirikisha wale ambao waligusana naye

Klabu hiyo imeongezea kwamba Rugani mwenye umri wa miaka 25 kufikia sasa hajaonesha dalili za ugonjwa huo.

Michezo yote nchini Italia imeahirishwa hadi Aprili 3 huku taifa hilo likijiweka katika karantini kutokana na mlipuko huo wa coronavirus.

Rugani ameichezea klabu yake mara saba pekee msimu huu na hakutumika katika mechi ya Juventus dhidi ya Intermilan ambayo klabu hiyo iliibuka na ushindi wa 2-0 katika mechi iliochezwa bila mashabiki siku ya Jumapili.

Mechi ya Inter iliotarajiwa kucheza dhidi ya Getafe katika michuano ya Europa siku ya Alhamisi pia imeahirishwa.

Rugani ameshinda mataji manne ya ligi ya Italia akiichezea Juventus na aliichezea Italia mara saba, mara ya mwisho ikiwa 2018.

Siku ya Jumapili alichapisha picha mtandaoni katika chumba cha maandalizi cha Juve akisherehekea ushindi wa klabu hiyo dhidi ya Inter pamoja na wachezaji wenzake.

Italia imerekodi visa 12,000 vya maambukizi na vifo 827 kutokana na virusi hivyo.

Wakati huohuo mechi kati ya Arsenal na Manchester City imeahirishwa baada ya kuwepo kwa hofu ya virusi vya corona, huku baadhi ya wachezaji wa Arsenal wakiamua kujitenga baada ya mmiliki wa klabu ya Olympiakos Evangelos Marinakis kupatikana na virusi hivyo.

Arsenal inasema kwamba Marinkis mwenye umri wa miaka 52 alikutana na baadhi ya wachezaji wake wakati Arsenal walipokuwa wenyeji wa mechi na klabu hiyo katika kombe la Europa wiki mbili zilizopita.
Marinakis ambaye pia anaimiliki klabu ya ligi ya daraja la kwanza nchini England Nottingham Forest alisema siku ya Jumanne kwamba amepatikana na virusi vya corona.

Arsenal inasema kwamba baadhi ya wachezaji wake walikutana na mmiliki wa klabu hiyo ya Olympiakos.

APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini