KADA MWINGINE CHADEMA ATIMKIA NCCR-MAGEUZI, AKERWA NA KUTOTHAMINIWA KWA MWANAMKE | ZamotoHabari.

Charles James, Globu ya Jamii

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezidi kukimbia na wanachama wake baada ya aliyekua kiongozi wa chama hicho kujiengua ndani ya chama hicho na kujiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi.

Ndiholeye Kifu ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo Ukatibu Mwenezi na baadae Mwenyekiti wa Bawacha wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Chadema (Chaso) kutoka Chuo Kikuu cha Katoliki Mwenge mkoani Kilimanjaro amejiuzulu kwa kile alichoeleza kutoridhishwa na mwenendo wa chama chake.

Amesema baada ya kutafakari kwa muda mrefu amebaini Chadema ni chama ambacho hakizingatii utu wa mwanamke na wala hakuna usawa wa kijinsia ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma, Ndiholeye amesema ni jambo la kushangaza pia kuona Chadema inayodai Tume huru ilihali yenyewe ndani ya chama hakuna Uhuru wa kugombea na kuchagua.

" Hakuna uhuru pale. Nafasi za juu za uongozi ni kama zina watu wake ambao wameshapangwa kuzishika. Wewe mwingine ukijitokeza kuchukua fomu ugombee unaambiwa acha hiyo nafasi ina mtu. Halafu tukitoka nje tunadai tume huru.

Nafasi ya mwanamke Chadema ipo kwenye Bawacha na viti maalum tu. Ukiangalia kuna kanda 10 lakini makatibu wake wote ni wanaume, kwenye zile nafasi sita za juu za uongozi zote wapo wanaume inamaana hakuna mwanamke ambaye anaweza kuongoza au ni kudharauliwa? Amehoji Ndiholeye.

Amesema ameamua kujiunga na NCCR kwa kuwa ni chama kinachoamini kwenye kujenga usawa na utu huku akiamini pia ni sehemu ambayo inaweza kumlea kama kijana katika kutimiza malengo yake ya kisiasa tofauti na Chadema.

Ameongeza kuwa chama cha siasa kinazaliwa, kinakua kikubwa na kinakufa, hivyo Chadema ipo katika hatua zake za kufa kutokana na mwenendo wao ambao umekua hauridhishi.

" Haiwezekani kila siku viongozi wake mbalimbali wanaondoka na kujiunga na vyama vingine lakini hawashtuki, wanaona sawa tu. Nakuhakikishia wasipofanya mabadiliko kwenye chama chao basi kinaenda kufa muda siyo mrefu," Amesema Ndiholeye.

Aliyekua kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Ndiholeye Kifu akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma alipokua akitangaza uamuzi wake wa kujiondoa Chadema na kujiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini