VIJANA WANAOVUTA GUNDI WAZIDI KUSHAMIRI DODOMA, WANANCHI WAFUNGUKA | ZamotoHabari.


Charles James, Michuzi Globu

PAMOJA na Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi lakini bado idadi ya vijana wanaotumia dawa za kulevya aina ya gundi imezidi kuwa tatizo kwa wananchi wa jiji hilo.

Vijana hao wamekua wakishinda na kuzagaa katikati ya Jiji maeneo ya viwanja vya Nyerere ambapo wamekua wakicheza kamari, kusumbua wananchi wanaopita, wanafunzi na zaidi wakivuta gundi hadharani.

Globu ya Jamii imefanya uchunguzi wake na kugundua kuwa umri wa vijana hao ni kuanzia miaka tisa hadi 21 na wamekua pia wakiiba vitu kwenye magari yanayopaki maeneo ya Nyerere Square lakini pia wamekua wakiwasumbua wanafunzi wanaokatiza karibu yao.

" Kwa kweli hawa watoto ni wasumbufu sana, mimi walishawahi kuniibia pochi kwenye gari yangu, lakini hata ukiwakamata ukawapeleka Polisi bado haisaidii, nafikiri uongozi wa Jiji la Dodoma ungeweka namna nzuri ya kuhakikisha vijana hawa wanasaidiwa kuachana na tabia hii.

Ukitazama umri wao wengi ni bado watoto wadogo, walipaswa kuwa shule kitendo cha kuwakuta maeneo haya maana yake wazazi wameshindwa kuwasimamia na kuwalea katika namna inayotakiwa. Au ukichunguza zaidi unagundua ni wale watoto ambao wazazi walitengana," Amesema Abdallah Sufiani ambaye ni mkazi wa Dodoma.

Mwanzoni mwa mwaka jana, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe Patrobas Katambi alifanya msako wa kuwakamata vijana hao na kuwapeleka katika vituo vya kulea waathirika wa dawa za kulevya lakini baadae vijana hao walitoroka na kurudi tena mtaani kuendelea na utumiaji wa gundi.

Akizungumzia wimbi la vijana hao, mwananchi mwingine, Joseph Kindi amesema ni wajibu wa serikali, wadau wa maendeleo ya jamii, wazazi kushirikiana katika kutokomeza tatizo hilo kabla halijazidi kuwa kubwa.

" Hawa watoto ni wadogo sana, tukiwaacha na kuchukulia kawaida kuna hatihati ya baadae Dodoma kuwa na mateja kama Dar. Ni vema kuja na mkakati wa pamoja kama Jiji kuhakikisha tunaokoa vijana hawa ambao ni nguvu kazi ya Taifa.

Hatuwezi kumuachia DC pekee yake apambane nao, wazazi ni jukumu letu kuwalea watoto hawa, wadau wa maendeleo ya jamii, wanaharakati wa haki za watoto wote kwa pamoja tuje na mpango thabiti wa kupunguza changamoto hii," Amesema Kindi.
 Baadhi ya kundi la vijana wanaovuta gundi jijini Dodoma wakiwa wanacheza kamari maeneo ya Nyerere Square ambapo ni katikati ya Jiji la Dodoma. Chupa zinazoonekana ndizo wanazoeka gundi ndani yake na kuvuta.
 Hawa ni vijana wanaotumia dawa za kulevya aina ya gundi. Mmoja mwenye kofia akiwa anavuta gundi hiyo hadharani na mwingine akiwa anaomba kwa wenye magari.
 Huyu nae ni miongoni mwa watumiaji wa dawa za kulevya kama inavyoonekana hapo akiwa ameshika chupa yake yenye gundi ndani.
 Hawa ni vijana wanaotumia dawa za kulevya aina ya gundi wakiwa wanazozana. Huyo wa kushoto akiwa amebeba chupa mbili zenye gundi.
Vijana wanaovuta dawa za kulevya aina ya gundi jijini Dodoma wakiwa wamekaa barabarani wakicheza kamari hadharani.
 


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini