KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YATOA USHAURI KWA SERIKALI KUHUSU KUVILINDA VIWANDA VYA VIFAA VYA UMEME | ZamotoHabari.

Na Mwandishi Wetu, Michuzi Globu ya jamii

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kuvilinda viwanda vya uzalishaji wa vifaa vya umeme vilivyopo nchini ili kuongeza tija na ufanisi wa viwanda hivyo vilivyopewa jukumu la kuzalishaji vifaa hivyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme inayoendelea nchini.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo kutembelea kiwanda cha uzalishaji wa vifaa vya umeme na Transfoma cha AFRICAB kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dustan Kitandula, pamoja na ushauri huo pia ameiomba Serikali kuhakikisha malipo ya wenye viwanda hivyo yanafanywa kwa wakati ili kuwapa nguvu katika uzalishaji.

Amesema ili viwanda hivyo vitekeleza majukumu yake ipasavyo hasa wakati huu ambao vimepewa jukumu la kuzalisha vifaa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi iliyopo chini ya Wakala wa Umeme Vijijini(REA) na Shirika la Umeme nchini (TANESCO), na kwamba kuna kila sababu ya kuhakikisha inadhibiti uingizwaji wa vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi ili kuepusha kuharibu soko la ndani sambamba na kumlinda mzawa.

“Sote tumeshuhudia kazi nzuri inayofanywa na kiwanda hiki na vingine ambavyo tumepata nafasi ya kuvitembelea, vimeonyesha kuwa na uwezo mkubwa katika uzalishaji wa vifaa hivyo na kuondoa ulazima wa uingizwaji wa vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi” alisema Kitandula.

Aidha alikipongeza kiwanda hicho cha AFRICAB kwa kasi yake ya uzalishaji wa vifaa hivyo vya umeme kuendana na kasi ya wakandarasi waliopo katika jukumu la utekelezaji wa miradi hiyo ya Serikali akiwataka pia kuhakikisha ‘wanajiongeza’ katika kutafuta masoko nje ya nchi baada ya kuelezwa mafanikio yaliyofikiwa na kiwanda hicho kwa sasa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, pamoja na kukipongeza kiwanda hicho, alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha wanakomesha uingizwaji wa vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi wakati huu ambapo tayari imeshapiga marufuku uingizwaji wa nyaya kutoka nje ya nchi.

“Kwa sasa tumeeunda kamati kuona kama uzalishaji wa vifaa vya uunganishaji wa umeme majumbani kama unatosheleza kutoka katika viwanda vetu, tukiona kuna matokeo mazuri basi tutazuia visiingizwe kutoka nje ya nchi, lakini napenda nikiri kuwa viwanda vyetu kwa sasa vinafanya kazi nzuri sana ni vyema tukavipongeza kwa hatua hiyo” alisema Mgalu.

Aidha amesisitiza Serikali itazidi kuwa karibu na wenye viwanda hivyo ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo hususani wakati huu vinapotekeleza majukumu makubwa ya uzalishaji wa vifaa hivyo kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo ya kimkakati inayofanywa na Serikali.

Awali Mkurugenzi wa Kiwanda hicho cha AFRICAB Mohammed Ezzi alisema mbali na uzalishaji wa nyaya na vifaa vingine vya umeme wa majumbani,kiwanda hicho kinazalisha Transfoma alizodai kuwa zina uwezo wa juu tofauti na zinazoingizwa kutoka nje ya nje na kusisitiza kuwa uzalishaji wake kwa sasa umezidi kiwango cha mahitaji yake hapa nchini.

Ameiomba Kamati hiyo na Serikali kuwaamini na kuachana na mtazamo hasi kutoka kwa baadhi ya watu wanaofikiri kuwa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani havina ubora ikilinganishwa na vifaa vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi, jambo alilosema pia linawavunja moyo wazalishaji wa ndani.

Amesema kiwanda hicho kwa sasa mbali na kusambaza bidhaa zake hapa nchini, pia wanayo masoko katika nchi za Congo, Zambia, Malawi Uganda pamoja na Kenya.
 
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula(aliyenyoosha mkono) akifafanua jambo baada ya kutembelea kiwanda hiho akiwa na wajumbe wa kamati hiyo.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini