MBUNGE MAVUNDE ASAIDIA UPATIKANAJI WA VIFAA TIBA 100 KWA WATU WENYE ULEMAVU JIJINI DODOMA | ZamotoHabari.

Charles James, Michuzi TV

KATIKA kuhakikisha anatekeleza azma ya Rais Magufuli ya kuwahudumia wananchi wanyonge, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amezindua rasmi kambi ya upimaji wa tiba saidizi vya miguu ya bandia kwa watu wenye ulemavu.

Uzinduzi huo umefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na huduma hiyo itakua ikitolewa kwa wananchi wote kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Dodoma na maeneo jirani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe Mavunde amesema vifaa hivyo vitakua ni msaada kwa watumiaji 100 ambao wamepatiwa na kwamba ataendelea kushirikiana na watu wenye mahitaji katika kutatua changamoto zao mbalimbali.

Mhe Mavunde ameishukuru Taasisi ya People Empowerment Foundation (PEF) iliyo chini ya kwa mchango mkubwa wa huduma ya upimaji na baadaye kutoa vifaa tiba saidizi vya miguu ya bandia kwa takribani wahitaji 100 ambao katika hali ya kawaida wengi wao wasingekuwa na uwezo wa kununua miguu bandia ambayo inauzwa kuanzia Sh 800,000 hadi Sh 1,000,000.

" Kwa kweli niwashukuru sana ndugu zetu hawa wa PEF kwa kutushika mkono, mmewainua wananchi hawa kwa namna leo mlivyojitoa kwenu, niwahakikishie kuwa mimi kama Mbunge wa wananchi hawa nimeguswa kwa mchango wenu na ninawashukuru sana.

Niwaombe pia taasisi na mashirika mengine kuguswa na jambo hili ambalo PEF wamelifanya kwetu, hata kama siyo kwa hawa ndugu zetu wenye ulemavu basi kuna uhitaji katika maeneo mengine niwaombe sana mjitokeze katika kuwasaidia wananchi wetu wanyonge," Amesema Mavunde.

Nae  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Sameer Santoji amesema taasisi yake imejipanga kuwawezesha watu wenye ulemavu hasa kwenye mahitaji yao ya vifaa tiba hivyo wameamua wenyewe kuanza kutengeneza viungo hivyo ili kurahisisha upatikanaji wake.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Ibenzi Ernest amepongeza juhudi zinazofanywa na Mbunge Mavunde katika kuwahudumia wananchi wenye uhitaji  ambapo hii ni mara ya tatu anawahudumia makundi maalum kwa kuwatafutia misaada mbalimbali nje ya utaratibu wa Hospitali.
 Mmoja wa wananchi wenye ulemavu ambao amejitokeza kwenye uzinduzi wa kambi ya upimaji wa tiba saidizi vya miguu ya bandia kwa watu wenye ulemavu akiwekewa vifaa tiba kwenye mguu wake.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma, Mhe Anthony Mavunde akizungumza na wananchi mbalimbali waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kambi maalum la upimaji wa tiba saidizi vya miguu ya bandia kwa watu wenye ulemavu.

 Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe Anthony Mavunde akisalimiana na wananchi wenye ulemavu ambao waliojitokeza katika uzinduzi wa kambi hilo sambamba na kupatiwa vifaa tiba.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini