MKOA WA GEITA WAPONGEZWA KWA KUWA WABUNIFU KWENYE MIUNDOMBINU YA ELIMU | ZamotoHabari.


NAIBU Katibu Mkuu anayeshughulika Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Gerald Mweli amefurahishwa na ubunifu wa kutumia tofali mfungamano (Interlock) kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa katika kukabiliana na mrundikano wa wanafunzi katika shule za Mkoa wa Geita.

Mweli ameonyesha furaha yake wakati wa ziara ya kikazi Mkoani humo iliyokua na lengo la kukagua miundombinu ya Elimu iliyojengwa na inayoendelea kujengwa pamoja na  kupokea changamoto za walimu na kuzitolea ufafanuzi.

Akiwa Mkoani Geita Mweli aliweza kujionea namna ambavyo Mkoa huo umejiongeza kwa kupeleka mashine za kufyatulia matofali mfungamano katika Halmashauri zote na kujenga darasa la mfano kwa kutumia tofali hizo katika shule ya sekondari nyanza.

Akikagua darasa hilo Mweli amesema ubunifu ni wa kuigwa na Mikoa mingine sababu umeonyesha umakini wa hali ya juu wa viongozi wa Mkoa wa Geita, uzalendo, kujitoa  na kupunguza changamoto ya uhaba wavyumba vya madarasa katika shule za Serikali.

“Nimefarijika sana kuona darasa limekamilika kwa kutumia matofali haya ambayo ni ya gharama nafuu kwani sasa gharama za ujenzi wa chumba cha darasa kwa mkoa wa Geita imeshuka kutoka shilingi milioni 20 mpaka kufikia milioni 11 tu hili ni jambo zuri na la mfano nawapogeza sana Geita” Amesema Mweli.

Mweli ameongeza kuwa Geita ni miongoni mwa mikoa yenye uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa na shule zake nyingi zina wanafunzi wengi mno kiasi kwamba hata ufundishaji wa wanafunzi hao umekuwa changamoto lakini viongozi wa mkoa huu wamejiongeza na kuja na ubunifu huu wa kupunguza gharama za ujenzi kwa kutumia matofali mfungamano.

" Niwapongeze sana viongozi wote ndani ya Mkoa kuja na mpango huu ambao sasa tutaweza kujenga vyumba vingi zaidi na kupunguza changamoto ya mrundikano wa wanafunzi, huu ni ubunifu mkubwa na unapaswa kuigwa na Halmashauri zingine," Amesema Mweli.

Akizungumzia mpango huo Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Robert Gabriel amesema wao kama viongozi hawataki mpaka waagizwe kutoka juu wanachofanya ni kubainisha changamoto walizonazo, wanaweka mikakati mapema, na kuanza kutekeleza kwa wakati na kutatua changamoto zao.

“Mahitaji ya vyumba vya madarasa katika Mkoa wetu ni zadi ya vyumba 9000 na tunategemea wanafunzi wengine watamaliza shule hivi karibuni hivyo mahitaji yataongezeka zaidi ya sasa tunajiandaa mapema kukabiliana na mahitaji tuliyonayo” Amesema Mhe Gabriel.

Ameongeza kuwa mashine hizo za kufyatulia matofali ya mfungamano zilikuwepo tangu zamani lakini hazikuwa zikitumika hivyo akaona ni muda sasa kuzigawa kwa kila halmashauri kuwaelekeza namna ya kuzitumia ili nao waanze kufyatua matofali ya kujengea madarasa.
 Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Gerald Mweli akiwa na viongozi wa Mkoa wa Geita kwenye mkutano wa pamoja na watumishi wa halmashauri zote za Mkoa huo wenye lengo la kutatua changamoto walizonazo kwenye sekta ya elimu.
 Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Robert Gabriel (katikati) akitoa maelezo kwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Gerald Mweli (kulia) wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya elimu kwenye halmashauri za Mkoa huo.
 Muonekano wa jengo la darasa la mfano kwenye Shule ya Sekondari ya Nyanza lililojengwa kwa kutumia matofali mfungamano ambalo Naibu Katibu Mkuu Tamisemi ameridhishwa nalo.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini