UHITAJI MKUBWA WA MAZAO YA MBOGAMBOGA JIJINI MBEYA UMECHANGIA KASI YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI | ZamotoHabari.


Katika picha, mkulima wa zao la mahindi Bi. Joyce Nassoro akionyesha shamba lake la mahindi yatokanayo na kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Uyole Jijini Mbeya , halipo katika picha, ambapo mkulima huyo ameeleza kuwa ameweza kulima mahindi hayo kwa muda mfupi ambapo kwa sasa anayavuna kwa matumizi ya chakula cha nyumbani kwake.
Bibi Rose Samwande katika picha mkulima wa mbogamboga aina ya karoti katika Bonde la Uyole jijini Mbeya akionesha karoti ambazo zipo tayari kuvunwa kwa ajili kwenda sokoni na wakati pembeni yake linaonekana shamba ambalo lipo tayari kwa kilimo kingine cha zao hilo kinachotumia kilimo cha Umwagiliaji.
Bwana John Soda, mwenyekiti wa Umoja wa kilimo cha Umwagiliaji katika bonde la Uyole jijini Mbeya, akiongea kuhusu aina ya Mbegu ya karoti inayotumiwa na wakulima katika bonde hilo pamoja na madawa wanayotumia kuuwa wadudu, na ukulima wa aina hiyo ya mbogamboga kwa ujumla.
Zao la mbogamboga aina ya nyanya nalo hulimwa kwa wingi katika Bonde la Uyole jijini Mbeya, zao ambalo limekutana na changamoto ya kushambuliwa na wadudu maarufu kwa jina la kantangaze na kupelekea zao hilo kuadimika na kuongezeka bei sokoni.
Katika picha Shamba la Mahindi lililo tayari kwa kuvunwa katika Bonde la Uyole jijini Mbeya.



Na Mwandishi Wetu – Mbeya

IMEELEZWA KUWA, uhitaji mkubwa wa mazao ya mbogamboga katika Jiji la Mbeya na mikoa ya Jirani umechangia kwa kiasi kikubwa kasi ya kilimo cha Umwagiliaji katika skimu ya kilimo hicho ya Bonde la Uyole iliyopo Jijini Mbeya.

Hayo yameelezwa jana na Mwenyekiti wa umoja wa wakulima wa Umwagiliaji katika Bonde hilo Bw. John Soda, alipokuwa kizungumza na wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambapo amesema kuwa kutokana na uhitaji huo kuwa juu vijana wengi wamejikita katika shughuli hizo za kilimo rafiki na rahisi kisichotegemea mvua katika skimu hiyo yenye ukubwa wa eneo zaidi ya hekta mia moja (100).

Bwana Soda amesema kuwa, pamoja na mahitaji ya aina hiyo ya mazao kuwa juu kilimo hicho pia kimewasaidia wakulima kujipatia ajira inayowapelekea kujiongezea kipato binafsi, kupeleka watoto wao shule na kubadilisha hali ya maisha yao kwa ujumla.

Awali akiongea katika skimu hiyo ya kilimo cha umwagiliaji Bw. Soda aliishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kuboresha miundombinu ya umwagiliaji hususan mfereji wenye urefu wa mita elfu nne na mia tano (4,500) na kuiomba serikali kumalizia kusakafia kipande cha mita elfu moja na mia tano (1,500) zilizobakia katika eneo hilo la umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji.

Sambamba na hilo Bw. Soda aliiomba Serikali pia kusaidia katika upatikanaji wa soko la uhakika ambalo litapelekea mkulima kumfikia mnunuzi moja kwa moja bila kupitia dalali.

“Pamoja na hilo Tunaiomba pia Serikali kutusaidia kupata teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji inayotumia maji kidogo kama vile kilimo cha Drip Irrigation” Alisisitiza Bw. Soda.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini