MGONJWA wa akili kaunti ya Uasin Gishu nchini Kenya, ameponea kifo kwenye tundu la sindano baada ya ambulensi aliyoiiba kutoka Hospitali ya Rufaa ya Moi (MTRH) kugongana na lori la mafuta eneo la Marura kwenye barabara ya Eldoret-Iten.
Familia ya jamaa huyo mwenye umri wa miaka 30, ilimpeleka hospitalini hapo Machi 24 mwaka huu, na walikuwa wanasubiri ahudumiwe. Inasemekana kaka huyo alilichukua gari hilo la kubebea wagonjwa muda mfupi baada ya dereva aliyekuwa nalo kuliacha likiwa na ufunguo, huku injini yake ikiwa ingali inaunguruma.
Walioshuhudia kisa hicho walisema, dereva huyo alikuwa akikimbiza mgonjwa aliyekuwa mahututi kupata huduma hospitalini humo wakati jamaa huyo mwenye akili za kipunguwani aliruka ndani ya gari hilo na kutoweka nalo.
Baada ya kuliendesha gari hilo la hospitali ya kituo cha afya cha Kapteldon kwa hatua kadhaa, aligonga daraja la eneo la Marura akijaribu kukwepa kugongana na lori la kusafirisha mafuta.
Hata hivyo, dereva wa lori hilo alipoteza mwelekeo na kugonga pikipiki. Mshukiwa aliachwa na majeraha madogo huku dereva wa lori hilo akitoka bila jeraha lolote.
Ajali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa magari na kuwalazimu polisi kufika eneo hilo na kuiondoa ambulansi hiyo kutoka barabarani. Duru ziliarifu kwamba, mshukiwa alikuwa akihudumu kama dereva kabla ya kuanza kuwa tahira wakati alipopelekwa kupata matibabu katika hospitali hiyo.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments