Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akimsikiliza Meneja wa Karakana ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) Mbeya, Mhandisi Ezekiel Mong’ateko, wakati akimweleza hatua ya ukarabati iliyofikiwa katika karakana ya tazara mkoani Mbeya.
Muonekano wa moja ya Vichwa vya treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) vilivyokamilika baada ya kufungwa mashine ya kufua umeme (Tranction Motor), katika karakana ya Mamlaka hiyo Mkoni Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akizungumza na wafanyakazi wa karakana ya maelekezo Karakana ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) mkoani Mbeya (hawapo pichani) wakati alipokagua maendeleo ya ukarabati wa vichwa vya treni mkoani humo.
Muonekano wa vifaa vinavyofanyiwa ukarabati katika karakana ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) mkoani Mbeya.
Mafundi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) mkoani Mbeya, wakiendelea na ukarabati wa vichwa vya treni katika karakana hiyo mkoani humo. TAZARA iko katika hatua za mwisho za kukamilisha ukarabati wa kichwa cha tat umara baada ya kufunga traction motor mpya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akinawa mikono kama njia ya kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Korona katika Karakana ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) mkoani Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Karakana ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) Mbeya, Mhandisi Ezekiel Mong’ateko, mara baada ya kukagua vichwa viwili vya treni ya shirika hilo vilivyofungwa mashine ya kufua umeme (traction motor) mpya.
………………………………………………………………………………………………
Serikali ya Tanzania imetoa kiasi cha shilingi bilioni 10 ikiwa ni kuhakikisha inaifufua upya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuiongeza mtaji na kufikia lengo la kujiendesha kibiashara.
Akizungumza mkoani Mbeya mara baada ya kukagua vichwa viwili vilivyokamilika baada ya kufungwa mashine mpya za kufua umeme (traction motor) Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amesema kuwa kukamilika kwa ukarabati huo kutaongeza usafirishaji wa mzigo kwa mamlaka.
“Makusudi makubwa ya Serikali kuwekeza fedha hizi ni kuhakikisha mnafanya biashara na kurejesha mzigo wa tani milioni tano mnaotakiwa kuusafirisha kwa mwaka”, amesema Mhandisi Kamwelwe.
Kamwelwe amefafanua kuwa fedha hizo zilizotolewa zimeshanunua mashine mpya za kufua umeme takribani arubaini na mbili ambazo zitafungwa kwenye vichwa saba.
Meneja Karakana ya TAZARA mkoani humo, Mhandisi Ezekiel Mong’ateko, amesema mpaka sasa vichwa viwili vimeshakamilika na mwishoni mwa mwezi huu kichwa cha tatu kitakamilika ambapo kichwa kimoja kina uwezo wa kusafirisha tani laki mbili na nusu kwa mwaka.
“Kukamilika kwa vichwa hivi kutaongeza mzigo tunaotakiwa kuusafirisha kwa mwaka kwani kwa sasa mzigo tunasafirisha umepungua sana na hauzidi tani laki tatu, tunaishukuru sana Serikali kwa kuiwezesha mamlaka”, amesema Mhandisi Mong’ateko.
Mhandisi Mong’ateko ameongeza kuwa sambamba na ukarabati wa vichwa hivyo mkoani humo, Mamlaka inaendelea na ukarabati wa mabehewa katika karakana ya mamlaka jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha ukamilikaji wa vichwa hivyo unaendana na ongezeko la usafirishaji wa abiria na mizigo.
Kukamilika kwa ukarabati wa vichwa hivyo kutaongeza idadi ya vichwa kumi na tatu vilivyopo kwa sasa na kufikia vichwa 20 ambapo kila kichwa kina uwezo wa kubeba tani elfu thelathini.
Utoaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa makubaliano ya nchi Mbili ya Tanzania na Zambia ambazo kwa pamoja zilikubaliana kutoa bilioni 20 ambapo kila nchi ilitakiwa kuchangia bilioni kumi ili kuifufua upya mamlaka hiyo na kuiwezesha kujitegemea mara baada ya kushuka kwa usafirishaji kutokana na upungufu wa vichwa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments