Charles James, Michuzi TV
SIKU moja baada ya pazia la kampeni za uchaguzi mkuu kufunguliwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limetoa onyo kwa wale wote ambao wataleta vuruga au kuchochea uvunjifu wa amani kwa kipindi chote cha kampeni.
Onyo hilo imetolewa leo jijini Dodoma na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Gilles Muroto amesema wamejipanga kulinda amani na kukabiliana na wale wote wenye nia ovu ya kuanzisha vurugu.
Muroto amesema kama ilivyo kanuni na taratibu za jeshi hilo watahakikisha wanatoa ulinzi na usalama kwa muda wote wa kampeni za Urais, Ubunge na Udiwani kwa kila chama.
Amewataka wanasiasa wote watakaokuja kwenye kampeni mkoani Dodoma kuwa mstari wa mbele kuhamasisha ulindaji wa amani kwa wanachama na wafuasi wake na siyo kuwa sehemu ya vyanzo vya uvunjifu wa amani.
"Ndugu zangu wanasiasa niwasihi mtangulize maslahi mapana ya Nchi yetu pindi mtakapokuja Dodoma kwenye kampeni, Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma halitokua tayari kuvumilia vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani.
Tunategemea kusikia viongozi wa vyama wakiwa mstari wa mbele kuhamasisha utunzaji wa amani na tuwe wazi kabisa yeyote atakayeleta vurugu Dodoma atapata tabu sana." Amesema Kamanda Muroto.
Tayari Chama cha Mapinduzi kimeshatangaza kuzindulia kampeni zake za Urais jijini Dodoma ambapo mgombea wake na Rais Dkt. John Magufuli atazindua mkutano wake Jumamosi ya Agosti 29 mwaka huu katika Uwanja wa Jamhuri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma kuelekea uzinduzi wa kampeni za vyama vya siasa kwenye uchaguzi mkuu.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments