WAFANYABIASHARA WADOGO MWANZA WANUFAIKA NA MIKOPO NBC | ZamotoHabari.

Mfanya biashara wa jijini Mwanza Grace Meshaki maarufu kama Mama Kweka (katikati) akitoa ushuhuda mbele ya Mkurugenzi wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (Kulia) akieleza namna Benki ya NBC ilivyompatia mkopo mpaka sasa anamtaji wa Zaidi ya milioni 250 kutoka milioni 17 katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kutoa mikopo kwa wafanya biashara wadogo na kati iliyofanyika Gold Crest jijini Mwanza mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Meneja wa Tawi la NBC Mwanza, Rodgers Masolwa.
Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya taifa ya NBC hapa nchini Theobard Sabi akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa benki ya NBC Mkoa wa Mwanza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi kutoa mikopo nafuu kwa wafanya biashara wadogo na wakati jijini Mwanza

MFANYABIASHARA wa jijini Mwanza, Grace Kweka, ambaye amenufaika kupitia Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) amewataka watanzania kutoogopa kwenda kukopa benki kwa sababu taasisi hizo zimeanzishwa kwa ajili ya wananchi kukuza uchumi wao.

Akizungumza jijini hapa jana katika hafla maluum iliyoandaliwa na NBC na kukutanisha wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kutoka mikoa ya kanda ya ziwa ambao ni wanufaika wa benki hiyo, Kweka alisema alianza na mkopo wa Sh milioni 17 mwaka 2005 sasa amefikia kiwango cha Sh milioni 300.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara hasa wanawake wamekuwa wakiogopa kukopa katika taasisi za kifedha hivyo kujikuta wanashindwa kukuza mitaji yao wakati ipo benki maalum iliyolenga kuwainua wafanyabiashara wa ngazi zote.

“NBC ni benki yetu wafanyabiashara tuitumie vizuri ili tunufaike nayo riba zake ni rafiki, mimi nilianza nikiwa mjasiriamali lakini sasa ni mfanyabiashara wa kati, kikubwa ambacho nawasihi wafanyabiashara wenzangu ni uaminifu na kufanya biashara kwa kujituma ili kuweza kurejesha mkopo kwa wakati,”alisema na kuongeza.

“NBC ni benki inayosikiliza wateja wake, binafsi nimenufaika sana kupitia benki hii, hata kipindi cha corona niliwafuata nikawaeleza kwamba sasa sijaagiza mzigo kutoka nje tukazungumza wakanipunguzia riba kitendo hiki kinaonyesha kweli wamedhamiria kutuinua wafanyabiashara,”alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema lengo la benki hiyo ni kuhakikisha sekta binafsi inaendelea kupata sapoti ya kifedha kama mikopo na huduma za kibenki ili kuongeza uwezo wao wa kiuchumi na kukuza shughuli zao za uzalishaji hivyo kuwezesha uchumi wa nchi kuwa wa ushindani na kulifanya taifa kufikia uchumi wa kati.

Mkurugenzi wa Kitengo cha biashara kwa wateja wadogo na wakati kutoka NBC, Elvis Ndunguru, alisema lengo lakukutana na wafanyabiashara hao ni kuzungumza nao kuhusu bidhaa za kibenki ambazo benki hiyo inazitoa ili kuwawezesha wajasiriamali kukuza shughuli zao za kiuchumi.

“Leo tutawaeleza wafanyabiashara kuhusu bidhaa za mikopo tunazozitoa ambazo zimeondolewa dhamana kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara na makampuni makubwa,” alisema.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini