SPIKA NDUGAI AZINDUA KAMPENI JIMBO LA 'RAIS' AMUOMBEA KURA MAGUFULI NA NDEJEMBI | ZamotoHabari.


Charles James, Michuzi TV

Kampeni za Ubunge Jimbo la Chamwino mkoani Dodoma zimezinduliwa leo rasmi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye amemuombea kura mgombea Urais wa chama hicho, Dk John Magufuli, mgombea Ubunge, Deo Ndejembi pamoja na madiwani wote.

Akizungumza wakati wa kumnadi Ndejembi, Spika Ndugai amesema miaka minne ambayo mgombea huyo alihudumu kama Mkuu Mkuu wa Wilaya ya Kongwa ni kigezo kimojawapo ambacho kinamfanya amuombee kura za Ubunge wa Chamwino kwa kuwa anauamini utendaji kazi wake.

Amesema maendeleo ambayo Kongwa imeyapata kwa muda mfupi licha yeye kuwa Spika lakini yamesimamiwa kwa ustadi mkubwa na Ndejembi na hivyo kuwataka wananchi wa Chamwino kumchagua ili aweze kuwaharakishia maendeleo kama alivyofanya Kongwa.

" Ndugu zangu wa Chamwino mmepata mgombea Ubunge makini na mwenye uwezo mkubwa wa kazi, niwasihi msimuachie huyu kijana, namfahamu kwa sababu amekua DC Kongwa na amefanya kazi kubwa, ninaamini ni mtu sahihi mwenye kuwavusha hapa na kuwapeleka mbali zaidi.

Jimbo hili ndio Ikulu ilipo, ndipo Rais anapoishi hivyo mnahitaji Mbunge mwenye kuendana na spidi ya Rais Magufuli mwenyewe, Mbunge ambaye atawapa hadhi ya jimbo la Ikulu, mtu huyo ni Ndejembi nendeni mkampigie kura nyingi Rais Magufuli, Ndejembi na madiwani wote wa CCM," Amesema Spika Ndugai.

Kwa upande wake mgombea Ubunge, Deo Ndejembi amewaomba wananchi wa Chamwino kumchagua kwa wingi Dk Magufuli awe Rais kwa miaka mitano mingine ili waweze kushirikiana kushughulika na changamoto zinazowakabili ikiwemo kero ya Maji na miundombinu ya Barabara.

" Niwaahidi miaka minne ya u-DC Kongwa imenipa uzoefu mkubwa wa kuwatumikia wananchi, ninaamini kwa pamoja tunaweza kuifanya Chamwino kupaaa zaidi na kuendana na hadhi ya Ikulu, ahadi yangu kwenu ni unyenyekevu, uchapakazi na uadilifu katika kuwatumikia.

Lakini ili tumpe ari zaidi Dk Magufuli ya kuipeleka mbele kimaendeleo Chamwino ni lazima tumpigie kura nyingi za Ndio ifikapo Oktoba 28, yeye ni mkazi mwenzetu wa hapa na mpiga kura wa Chamwino tumpigieni kura za kishindo hadi wapinzani wakome, " Amesema Ndejembi.

Amemuahidi Mjumbe wa Kamati Kuu, Spika Ndugai kuwa watashirikiana na watia nia wenzake wa ubunge na madiwani pamoja na viongozi wa chama wilaya katika kuzisaka kura za mgombea Urais, Mbunge na Madiwani na lengo lao ni Chamwino kuongoza kwa kura za Magufuli Oktoba 28 mwaka huu.

Uzinduzi huo wa kampeni umehudhuriwa pia na mgombea ubunge wa Kibakwe, George Simbachawene, mgombea Ubunge jimbo la Mvumi, Livingstone Lusinde, Wabunge wateule wa Viti Maalum Wanawake, Mariam Ditopile na viongozi wa ngazi ya Mkoa na Wilaya.
 Umati wa Wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za Ubunge jimbo la Chamwino wakimuaga mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM, Deo Ndejembi.
 Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Spika wa Bunge, Job Ndugai (kushoto) akimkabidhi Ilani ya chama hicho Mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Chamwino mkoani Dodoma, Deo Ndejembi wakati wa kampeni hizo leo katika Kata ya Dabalo.
 Mgombea Ubunge Jimbo la Chamwino kupitia CCM, Deo Ndejembi akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni zake leo
 Spika wa Bunge, Job Ndugai akihutubiwa wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za ubunge Jimbo la Chamwino mkoani Dodoma na kumnadi mgombea wake, Deo Ndejembi.
 Wananchi wakifuatilia mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Ubunge Jimbo la Chamwino katika Kata ya Dabalo
 Muonekano wa wananchi na wakazi wa Jimbo la Chamwino waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za Ubunge ambapo mgombea wa CCM, Deo Ndejembi amezindua kampeni zake.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini