WATUMISHI WIZARA YA KATIBA NA SHERIA WASISITIZWA KULINDA MALI ZA UMMA | ZamotoHabari.

WATUMISHI wa Wizara ya Katiba na Sheria wametakiwa kulinda mali za umma kama za kwao binafsi ili ziweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.

Maelekezo hayo yametolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo wakati akifungua mkutano wa Baraza hilo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro jijini Arusha.

“Watumishi wote tunatakiwa kulinda mali za umma kama za kwetu binafsi na kuzitumia kwa uangalifu mkubwa ili ziweze kudumu kwa muda mrefu”Alisema Prof. Mchome

Aidha, Prof. Mchome aliwaasa watumishi hao kuwa waadilifu kwa kutokunywa pombe wakiwa kazini, madereva wasibebe abiria njiani wanapokuwa safarini, pia watumishi wasiondoke na vifaa vya ofisi kwenda navyo nyumbani.

Mbali na hayo, Prof. Mchome alizitaka Idara na Vitengo katika Wizara hiyo kuwa na utaratibu endelevu wa kufanya vikao vya ndani mara kwa mara ili kubaini na kutatua changamoto zilizopo ndani ya Idara na Vitengo na kuepuka malalamiko kutoka kwa watumishi wa chini.

Alisema ,“Idara na Vitengo viwe na utaratibu endelevu wa kukaa vikao vya ndani ili kujua na kutatua changamoto mbalimbali zilizopo ndani ya Idara na Vitengo vyenu”.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ndg. Amon Mpanju aliwaeleza watumishi ambao ni wajumbe wa baraza hilo kurudi kwenye misingi ya utumishi wa umma na kuvaa ipasavyo kwa kuzingatia waraka wa mavazi uliotolewa na Manejimenti ya Utumishi wa Umma.

“Watumishi mnatakiwa mrudi kwenye misingi ya utumishi wa umma kwa kuzingatia waraka wa mavazi uliotolewa na menejimenti ya utumishi wa umma na sio mtumishi kuvaa mavazi yasiyostahili kwenye utumishi wa umma”, alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Katika mkutano huo wajumbe walipata nafasi ya kusikiliza mada mbili ambazo ni haki na wajibu wa mjumbe wa baraza la wafanyakazi pamoja na wajibu wa chama cha wafanyakazi katika baraza la wafanyakazi na mahala pa kazi iliyotolewa na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Manyara Bw. Samwel Said na mada ya pili ilikuwa ushirikishwaji wa wafanyakazi iliyotolewa na Afisa kazi Mkuu Mfawidhi Mkoa wa Manyara Bw. Perfectos Kimaty.

Awali kabla ya kuanza kwa mkutano huo wajumbe walipata nafasi ya kuchagua Katibu wa Baraza na Katibu Msaidizi kwani waliokuwepo wamemaliza muda wao. Katika uchaguzi huo Bi Basuta Milanzi alichaguliwa kuwa Katibu wa Baraza hilo baada ya kumzidi mshindani wake Bw. Felix Chakila ambaye alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi.

Mbali na kikao hicho, wajumbe walipata nafasi ya kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea hifadhi ya Ngorongoro na kujionea vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo ikiwemo mchanga unaohama.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome (wa pili kushoto) ambaye ni mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi la wizara hiyo akiongoza mkutano huo katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.Wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakiwa katika picha ya pamoja na Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Freddy Manongi baada ya ufunguzi wa mkutano huo.

Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakiwa mbele ya mchanga unaohama katika Hifadhi ya Ngorongoro.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini