Baada ya miezi kadhaa kupita tangu supastaa wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ atangaze kutoa misaada ya kodi kwa familia 500, hatimaye msaada huo umegeuka majanga kwa wakazi wanaoishi jirani na makazi ya jamaa huyo kufuatia kutapakaa kinyesi cha binadamu.
TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo makini kilicho jirani na makazi ya Diamond au Mondi maeneo ya Mbezi-Beach jijini Dar, kilipenyeza ubuyu kuwa hali ni mbaya kutokana na watu hao wanaoshinda kila siku kutaka msaada.
Supastaa wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
“Jamani ule msaada aliosema Diamond atautoa kwa watu umeleta shida hapa mtaani kwetu, hawa watu wanaohitaji msaada wamegeuka kero kwenye eneo hili, wanajisaidia hovyo; yaani vinyezi vimetapakaa nje hapa kama nini, tunaomba mje muangalie hali halisi ilivyo,” alisema jirani mmoja ambaye hakutaka jina lake lichorwe gazetini.
IJUMAA MZIGONI…
Baada ya kupewa ubuyu huo, Gazeti la IJUMAA huwa halilazi damu hivyo lilitimba nyumbani kwa Mondi na kukuta nyomi ya watu mbalimbali wakiwa nje ya geti wakisubiri kupewa chochote kitu.
WAFUNGUKA…
Gazeti la IJUMAA lilifanikiwa kuzungumza na baadhi ya watu hao ambapo kila mmoja alieleza changamoto yake.
Kuna baadhi walisema kuwa, tangu wamefika nyumbani hapo kwa Mondi, wana wiki kadhaa, lakini hawajawahi kukutana na msanii huyo.
“Mimi nimetokea Kigoma, kuna sehemu inaitwa Kibirizi, nilivyosikia lile tangazo kuwa Diamond atatoa msaada wa pesa, ndiyo nikaja huku Dar.
“Tangu nimefika nina miezi miwili, sina ndugu wa aina yeyote ile, ikifika usiku nahangaika sehemu ya kulala, kila tukijaribu kugonga getini kwake tunafukuzwa, ndiyo ikabidi nije kwa huyu mama (jirani wa Diamond) ndiye ametupa hifadhi ya kulala,” alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Steven Maisara.
MWINGINE WA MWANZA…
“Mimi natokea Mwanza, tumefika hapa muda mrefu sana, hatuna sehemu ya kula wala kulala, Mondi akitoka humo ndani yupo kwenye gari lake wala hatusikilizi, tunaomba mtusaidie tupate hata nauli ya kurudi nyumbani kwetu,” alisema mama mwingine aliyejitambulisha kwa jina Halima.
MKAZI WA ENEO HILO…
Mbali na wahitaji hao, mama mmoja mkazi wa eneo hilo ambaye hakuwa tayari jina lake liandikwe gazetini alitoa malalamiko yake kuwa, anaomba msanii huyo awaondoe watu hao katika eneo hilo kwani wamegeuka kuwa kero kubwa.
“Mimi nipo hapa mwaka wa 25 sasa, tangu huyu Diamond atoe kauli yake ya kusaidia watu, imekuwa kero kwa sisi tunaoishi hapa.
“Yaani kuna matukio ya kila aina. Mfano; wiki chache zilizopita kuna mama alibakwa hapa nje na baadhi ya hao vijana wanaojifanya wanahitaji msaada, tukiondoka majumbani mwetu tukirudi tunakuta wameiba vitu.
“Yaani ninakuambia hivi Mondi anatufugia wezi hapa maana siyo wote waliopo hapo wanahitaji msaada wengine ni wezi, jambo lingine ni kwamba hawa watu tangu wamefika hapa hawana sehemu za kulala hivyo ikifika usiku wanajisaidia hovyo tu, hali inayotufanya tukiamka asubuhi tunakuwa na kazi ya kuzoa vinyesi vyao utasema tunazoa vinyesi vya mbwa.
“Tumechoka jamani, tumechoka sana, kama hii hali ikiendelea tunaweza kukumbwa na magonjwa mengi ya mlipuko, tunaomba mumfikishie hizi taarifa Diamond awaondoe hawa watu hapa tumechoka,” alisema mama huyo.
SERIKALI YA MTAA…
Ili kupata mizani ya habari hii, Gazeti la IJUMAA lilifika mpaka kwa mjumbe wa eneo hilo, Sara Kimaro ambaye naye kwa upande wake alikiri kuliona tatizo hilo.
“Ni kweli wala siyo uongo, hilo tatizo lipo tena halijaanza leo wala jana, mfano huyo mama aliyebakwa tulifanikiwa kuwakamata vijana waliofanya unyama huo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
“Tumeshajaribu kadiri ya uwezo wetu kumtafuta huyo Diamond, lakini hatujawahi kufanikiwa. Kila tukifika pale nyumbani kwake tunaishia getini, haturuhusiwi hata kuingia ndani, ila maadam waandishi wa Gazeti la IJUMAA mmekuja, basi tutafanya jitihada za kumuandikia barua ili njia aliyoitumia kutangaza kuwa atatoa msaada ndio atumie njia hiyohiyo kuwatangazia kuwa amesitisha kutoa msaada wa pesa ili waondoke eneo lile.
“Pia siku nyingine akihitaji kusaidia watu, basi ashirikishe Serikali za Mtaa tutamsaidia au atumie njia nzuri ya kusaidia watu hao kwa sababu hivi anavyofanya sasa hivi anatuletea vibaka hapa,” anasema Mama Kimaro.
IJUMAA KWA MONDI
Baada ya kusikia malalamiko hayo, Gazeti la IJUMAA liligonga hodi nyumbani kwa Mondi ambapo walinzi walikuwa wakali kama pilipili kichaa.
“Hayupo nyumbani, nendeni ofisini kwake, haturuhusu mtu kusogelea geti…” Ilisikika sauti ya mlinzi ndani ya geti la Mondi.
Alipotafuta Mondi simu iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe kwa njia ya WhatsApp ulionesha ameusoma kwa kuweka tiki mbili, lakini hakujibu.
Kwa upande wao, mameneja wa Mondi, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ na Said Fella ‘Mkubwa’, waliomba kuachwa kwanza kwa kipindi hiki wakiwa bize na uchaguzi ambao umekaribia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu (Jumatano ijayo).
Tale anagombea Ubunge katika Jimbo ya Morogoro Kusini-Mashariki na Fella anagombea Udiwani katika Kata ya Kilungule, Temeke jijini Dar, wote kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
STORI: Memorise Richard na Jackline Wandiba, Ijumaa
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments